DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufungua mkutano wa Kimataifa wa Madini utakaowashirikisha washiriki 1,500 kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwemo mawaziri , mabalozi pamoja na watafiti
Mkutano huo wa siku tatu, utakaoanza Novemba 19 hadi 21, mwaka huu utafanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema,mkutano huo mbao unafanyika mara moja kila mwaka ni muendelezo wa jukwaa linalowakutanisha wadau wa madini kwa lengo la kushirikishana maarifa, ujuzi pamoja na washirki kujifunza sera za madini.
"Mkutano huu wa kimataifa wa madini unalenga kuweka msingi thabiti ya wadau , kauli mbiu ya mkutano huo ni 'Uongezaji thamani madini kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii,"amesema Mavunde.
Amesema, katika mkutano huo mada zipatazo nane zitatolewa na watoa mada wapatao 20 kutoka nje ya nchi na 30 kutoka hapa hapa nchini Tanzania ambao wamebobea kwenye sekta ya madini.
Amesema,mkutano huo utaambatana na usiku wa madini ambapo Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati,Dkt.Doto Biteko atakuwa mgeni rasmi ambapo lengo la usiku huo ni kutambua mchango wa wadau wa madini.
Amesema, katika usiku huo kutakuwa na onesho la bidhaa za madini ya vito pamoja na madini ya viwandani na ya ujenzi .
Aidha,mkutano huo utafungwa Novemba 21, mwaka huu na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi na kwamba maandalizi ya mkutano huo yapo katika hatua za mwisho.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 sekta ya madini ilikuwa kinara katika kuongeza fedha za kigeni ambapo dola bilioni 3.1, yalikuwa mauzo ya madini nje ya nchi na kwamba sekta ya madini ilichangia trilioni 2.1 kwenye pato ya taifa.
Amesema, mwaka 2024 Sekta ya Madini imetoa mchango kwa asilimia 9.0 kwenye pato la taifa na kwamba ifikapo mwaka 2025 ichangie kwa asilimia 10.