DAR-Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Bi. Zainab Kitima amewapongeza vijana wote waliojitokeza kugombea na kushinda nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa katika uchaguzi ulifanyika Novemba 27, 2024.
Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Bi. Zainab Kitima akiwashukuru watanzania kwa kuwaamini na kuwachagua vijana wasomi katika nafasi mbalimbali za uongozi wa Serikali za Mitaa kwenye uchaguzi ulifanyika Novemba 27, 2024.
Bi. Kitima ametoa pongezi hizo leo akiwa mjini Morogoro, ikiwa ni siku ya pili baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kutangaza matokeo ya jumla ya uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.
“Ninawapongeza vijana waliojitokeza kupiga kura na kugombea nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa katika maeneo mbalimbali nchini, hakika wametimiza haki yao ya kikatiba,” Bi. Kitima amesisitiza.
Bi. Kitima amewataka vijana wote ambao wameaminiwa na wananchi na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wanawatumikia wananchi kwa uadilifu na weledi ili kuwaletea maendeleo.
Bi. Kitima ameongeza kuwa, katika uchaguzi wa mwaka huu vijana wengi sana wamejitokeza kugombea nafasi za uongozi na ndio maana wameshinda, tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa inaaminika kwamba nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa ni kwa ajili ya wazee.
“Mwaka huu tumeona vijana wasomi wamegombea nafasi za ungozi wa Serikali za Mitaa na kushinda kwa kishindo, hivyo naishukuru jamii kwa kuwaamini vijana ili wapate fursa ya kutumia elimu yao katika kuwatumikia,” Bi. Kitima ameeleza.
Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Bi. Zainab Kitima akiendelea na majukumu ofisini kwake, mara baada ya kuwashukuru watanzania kwa kuwachagua vijana wasomi katika nafasi mbalimbali za uongozi wa Serikali za Mitaa kwenye uchaguzi ulifanyika Novemba 27, 2024.
Sanjari na hilo, Bi. Kitima ameipongeza Serikali kwa kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na wa haki, licha ya kuwepo na dosari chache zilizoripotiwa kwenye maeneo machache ambazo haziwezi kukosekana katika nchi yoyote ya kidemokrasia.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuvishirikisha vyama vyote vya siasa katika hatua na mchakato mzima wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024.
Jumla ya wananchi 26,963,182 wamepiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka huu uliofanyika Novemba 27, 2024.