MARA-Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza waombolezaji kuaga miili ya watu nane wa familia moja waliofariki kwa mafuriko katika Kata ya Nyamisangula, Mjni Tarime tarehe 24 Novemba, 2024 na kuwataka watu wote wanaoishi mabondeni kuhama ili kunusuru maisha yao.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya mafuriko hayo kuathiri eneo kubwa kandokando ya Mto Mori na kusomba nyumba nne na watu tisa kupoteza maisha huku watu wawili wakinusurika kifo na madaraja mawili yakiathirika katika eneo hilo.
“Tusikubali madhira kama haya yaendelee kutokea katika maeneo yetu, tunatakiwa kuchukua hatua sasa ili kunusuru maisha ya watu wengine na hususan watoto wadogo ambao sio rahisi kujiokoa wakati wa majanga kama haya,” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amekumbushia agizo lake alilolitoa Mei, 2024 kwa Halmashauri za Mkoa wa Mara kupanga matumizi bora ya ardhi na kuwahamasisha watu wote wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama na kama hawataki kuondoka kwa hiari Wilaya zitumie nguvu kuwahamisha.
Aidha, Mhe. Mtambi amewashauri wananchi kuwa na subira na kuchukua tahadhari wanapovuka mito au wanapopita sehemu zenye maji mengi ili kuweza kuokoa maisha yao na familia zao.
Mhe. Mtambi amesema watu waliopoteza maisha katika mafuriko hayo ni tisa ambapo miili minane imepatikana na mwili wa mtoto mdogo mwenye mwaka mmoja na nusu haujapatikana na manusura wawili ambao hali zao zinaendelea vizuri.
Kanali Mtambi amewapongeza wananchi kwa mshikamano na uzalendo waliouonyesha katika kutoa taarifa, kuokoa na kushiriki msiba na kuwataka kuendeleza mshikamano huu wa kindugu bila kujali kabila, kipato au dini ya mtu.
Mhe. Mtambi ameahidi ofisi yake itatoa shilingi milioni moja kwa ajili ya kujikimu kwa familia zote zilizoathirika na mafuriko hayo na kuongeza kuwa Serikali imetoa gharama zote za kufanikisha mazishi ya marehemu hao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele amewashukuru sana wananchi wa Wilaya ya Tarime kwa namna walivyotoa taarifa kwa viongozi na kushiriki katika shughuli ya uokoaji na kukiri kuwa bila ushiriki wa wananchi kazi hiyo ingekuwa ngumu sana.
Meja Gowele amewashukuru pia wananchi, viongozi na taasisi mbalimbali zilizotoa msaada wa hali na mali katika maafa hayo ikiwa ni pamoja na kuwahifadhi watu wa familia nne zilizoathirika na mafuriko hayo kwa kuwapa hifadhi, nguo na mahitaji mengine ya kibinadamu.
Amezishukuru familia za waathirika wa mafuriko hayo kwa ushirikiano walioutoa na kuwezesha taratibu za maandalizi ya mazishi kufanyika kwa wakati.
Mhe. Gowele amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika maafa hayo kwa kutoa maelekezo mbalimbali na ametoa pole nyingi sana kwa wafiwa wote na wote walioathirika na mafuriko hayo.
Mhe. Gowele amesema Ofisi yake kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Tarime itaendelea kuratibu misaada ya hali na mali kwa ajili ya waathirika wa mafuriko hayo ili kuhakikisha wanaanza maisha mapya sehemu salama.
Akizungumza katika msiba huo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara Mhe. Ghati Zephania Chomete ameipongeza Serikali kwa namna ilivyosimamia uokoaji hadi mazishi ya marehemu hao.
Mhe. Chomete ameahidi kutoa kilo 100 za mchele kusaidia familia zilizoathirika na mafuriko katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Vijijini Mhe. Mwita Waitara ameipongeza Serikali kwa namna ilivyoshirikiana na wananchi kuwaokoa waathirika wa mafuriko hayo na kuahidi kutoa gunia tatu za mahindi na mchele kilo 100.
Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara umetoa magodoro, vyakula na vifaa vya shule kwa ajili ya waathirika wa mafuriko hayo.
Mazishi hayo yamehudhuriwa pia na Kamati ya Usalama Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama Wilaya ya Tarime, viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara Mhe. Patrick Chandi, Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime.