REA kushirikiana na Njombe kusambaza mitungi ya gesi zaidi ya 13,000

NJOMBE-Mkoa wa Njombe umeahidi kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia 13,020 ili wananchi watumie nishati safi na salama.
Hayo yamezungumzwa Novemba 19, 2024 na Kaimu Katibu Tawala, Mha. Joseph Mutashubirwa baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REA katika mkoa huo iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Teknolojia Mbadala na Nishati Jadidifu, Mha. Advera Mwijage mkoani Njombe.

"Nawapongeza REA kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati hii ni salama na rafiki katika utunzaji wa mazingira yetu pamoja na afya za watumiaji wa nishati safi, "amesema Mha. Mutashubirwa.
Aidha, Mha. Mutashubirwa ameihakikisha REA kuwa mkoa huo utatoa ushirikiano na kuwahamasisha wananchi kuchukua mitungi ya gesi ya kupikia ili kuchochea uchumi na kutunza mazingira.

Kwa upande wake, Mha. Mwijage amezitaja wilaya zinazonufaika na mradi huo ni pamoja na Wilaya ya Njombe, Makete, Ludewa, na Wanging'ombe. "Kila wilaya itasambaziwa mitungi ya gesi 3,255 ya kupikia kwa wananchi kupitia kampuni ya Taifa Gas. Tunaendelea kuhamasisha kujitokeza kwa wingi kuchukua mitungi hii inayotolewa kwa bei ya punguzo ya asilimia 50,"ameeleza Mha. Mwijage.

Ameongeza kuwa, elimu ya matumizi sahihi ya nishati safi inaendelea kutolewa kwa Watanzania ili kuhamasisha na kuchochea jamii kutumia nishati safi na salama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news