ARUSHA-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imewanasua wakulima wa Maroroni huko Kata ya Nduruma Wilaya ya Meru mkoani Arusha katika kero ya ugawaji maji.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Bi.Zawadi Ngailo.
Amesema, TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka kwa mlalamikaji mkazi wa Njiro Arusha baada ya kuleta malalamiko yake.
Ni dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyohusisha wagawa maji katika mfereji wa Maroroni ambapo anafanya shughuli za kilimo cha vitunguu maji na vitunguu swaumu katika Kijiji cha Maroroni Kata ya Nduruma Wilaya ya Meru.
Ngailo amesema,katika kata hiyo kuna mfereji wa maji ambao unahudumia zaidi ya wanachama 400 ambapo kupitia kikao cha wananchi iliazimiwa kuwa wakulima wadogo wa eneo hilo watumie maji ya mfereji huo katika shughuli za umwagiliaji.
"Utaratibu wa kuwa mwanachama wa kilimo cha umwagiliaji katika Kitongoji cha Maroroi kilichopo katika Kata ya Nduruma ni kuwa unapaswa kuchangia kiasi cha shilingi 80,000 ambazo ni gharama za kusajiliwa na gharama za kupata huduma ya maji kutoka mfereji wa Maroroni kwa msimu mmoja.
"Sambamba na utaratibu huo, baada ya kutoa gharama hizo za usajili utaratibu wa kupata huduma ya maji ni mara mbili kwa wiki."
Aidha,uchunguzi ulibaini kuwa licha ya mlalamikaji kukidhi takwa hilo la kulipia gharama za kusajiliwa katika uanachama wa shughuli za kilimo Septemba 22,2024 watoa huduma ya maji wawili wa mfereji huo walimdai fedha kiasi cha shilingi 40,000 ikiwa ni kinyume na utaratibu.
"Kupitia uchunguzi huo, Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Arusha ilifanya mtego ambao ulifanikisha kukamatwa watuhumiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kiasi cha shilingi 40,000."
Amesema,washtakiwa hao wawili walifikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 40,000 kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura Namba 329 ya 2019.
"Watuhumiwa wote walikiri kutenda kosa hilo mbele ya Mahakama na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya shilingi 1,000,000 kila mmoja ambapo watuhumiwa hao walilipa faini ya shilingi 1,000,000 kila mmoja na kuachiliwa huru."
Aidha,kufuatia uchunguzi huo, washtakiwa hao wameondolewa katika zoezi la kugawa maji katika mfereji huo na kikao cha wanachama kimechagua wagawa maji wengine na utaratibu wa ugawaji wa maji unafuatwa na wakulima wananufaika na chanzo hicho bila ya malalamiko yoyote.
Tags
Habari
Kata ya Maroroni
Programu Rafiki ya TAKUKURU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)