RUVUMA-Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Tunduru imewahukumu Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Nambalapi, Bw. Shaibu Basi Swala, Mwenyekiti wa kijiji cha Nambalapi Bw. Shaibu Omary Shaibu na Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji Bw. Shabani Tukuru Mohamedi kulipa faini ya shilingi 800,000 kila mmoja au kwenda jela miaka minne.
Ni kwa kosa la kuomba na kupokea Rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1)(a)(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [Sura ya 329 mapitio ya mwaka 2024].
Hukumu dhidi ya Mtendaji wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kijiji na Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Nambalapi katika shauri la jinai namba 31695/2024 ilitolewa Novemba 25,2024 na Hakimu Mkazi Wilaya ya Tunduru Bi. Lilian Thadeus Haule (RM) mbele ya washtakiwa.
Ilieleza kwamba,washtakiwa walifikishwa mahakamani Novemba 7,2024 kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kiasi cha shilingi 1,750,000 ili waweze kumuuzia mkulima shamba anayeitwa Mhoja Seleli Mwabila, ambapo walimuuzia kwa makusudi eneo la msitu wa Hifadhi wa Kijiji cha Nambalapi kiasi cha hekari 75 kinyume na sheria.
Washitakiwa wametiwa hatiani na Mahakama imewahukumu kulipa faini kiasi cha shilingi 800,000 kila mmoja au jela miaka minne.
Aidha,washtakiwa wamelipa faini kila mmoja kiasi cha shilingi 800,000.
Shauri liliendeshwa na Waendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,Bw. Havin Charles, Bi. Nuru Muyinga na Bw. Mwinyi Yahaya.