ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeongeza bajeti ya Maendeleo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutoka TZS bilioni 83.2 mwaka 2021/22 hadi kufikia TZS bilioni 518 mwaka 2024/2025.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Novemba 1, 2024 alipofungua Skuli mpya ya Ghorofa tatu, ya Sekondari ya Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini, Pemba ikiwa ni mwendelezo wa kupongeza miaka minne ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya nane anayoiongoza.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema, bajeti hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 522.6 ambayo Imesaidia kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi ya kimkakati, inayolenga kuboresha elimu ya watoto na kuweka misingi imara ya maendeleo ya muda mrefu kwa Taifa.
Halikadhalika akiizungumzia bajeti ya Elimu ya Juu, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka TZS bilioni 11.5 kwa mwaka 2021/2022 hadi bilioni 33.4 mwaka 2024/2025 bajeti iliyoongeza idadi ya wanafunzi kutoka 4289 hadi kufikia 6,060.