ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuanzia sasa Serikali itawafidia nyumba bora wananchi wanaotoa maeneo yao kupisha miradi ya maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa, Serikali imedhamiria na jukumu la msingi la kuhakikisha wananchi wanapata makaazi bora ya kuishi.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Novemba 23,2024 alipozindua Mradi wa mauzo wa Nyumba za Chumbuni zinazojengwa na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) katika Ukumbi wa Mikutano Hoteli ya Amani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amefahamisha kuwa, jitihada hizo zimekuwa endelevu kwa awamu tofauti zilizoanza baada ya Mapinduzi ya Januari 1964 chini ya uongozi wa Hayati Abeid Aman Karume.
Rais Dkt.Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kutafuta fedha zaidi za kuendeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa nyumba za makazi maeneo mbalimbali.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ametoa rai kwa wananchi kuhamasika kununua nyumba hizo ili kuwa na makazi bora na ya kisasa.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kufarijika na kasi ya utendaji wa Shirika la Nyumba hivi sasa kwani limekuwa likitekeleza miradi yenye tija badala ya kushughulikia migogoro ya nyumba kwa muda mrefu.
Akitoa taarifa ya kitaalamu ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzbar, Sultan Said ameeleza kuwa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025 ya kuimarisha nyumba za makazi.
Ameeleza, mradi wa Chumbuni utakuwa na nyumba 3,000 na shirika linakusudia kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya ujenzi wa nyumba maeneo ya Kikwajuni, Kwa Mchina Unguja, Kisakasaka na Mabaoni Mfikiwa Pemba.