Serikali kuboresha mazingira ya biashara

NA EVA NGOWI
WF

SERIKALI imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali kama Utalii, Kilimo, Madini, Viwanda, Uvuvi na Ufugaji, kulinda viwanda vya ndani, kuvutia mitaji na uwekezaji nchini, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani, kuchochea ulipaji kodi kwa hiari na kuboresha usimamizi na ukusanyaji wa kodi, ada na tozo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama, akitoa ufafanuzi wakati wa Kongamano la Kodi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali (hawamo pichani) lililofanyika jijini Arusha.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama, wakati wa zoezi linaloendelea la kupokea na kukusanya maoni kwa wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali kwenye Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha.Arusha.
Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama, (wa kwanza kushoto) akiandika maoni yaliyokuwa yanatolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Usafirishaji Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na Manyara Bw. Locken Massawe, (aliyesimama), Kongamano lililofanyika Jijini Arusha.

Bw. Manyama alisema mojawapo ya maoni yaliyotolewa mwaka jana yalifanyiwa kazi ikiwemo kusamehe VAT kwenye Vifaa na Mitambo ya kuchakata na kuhifadhi mazao ya nyuki, kusamehe VAT kwenye kwenye chai inayotengenezwa ndani ya nchi (Local Blended Tea) pamoja na Kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye madini ya dhahabu yatakayouzwa kwa Viwanda vya Kusafisha Madini ya Dhahabu nchini.
Mtunza Hazina wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Arusha, Bi. Ester Msule, akitoa maoni yake kuhusiana na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha.

Alisema, Serikali pia imetoa unafuu wa kutolipa kodi ya mapato mbadala (Altenative Minimum Tax) kwenye kampuni zinazochakata mazao ya chai, kupunguza ushuru wa bidhaa kutoka shilingi 63.80 hadi shilingi 56 kwa lita ya maji ya kunywa yaliyosindikwa, kuanzisha vyanzo kwa ajili ya kugharamia Bima ya Afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na kuongeza ushuru wa forodha kwenye baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.
Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama, akitoa ufafanuzi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali (hawapo pichani) katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha, kulia kwake ni Afisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Arusha Bi. Sia Maruda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Usafirishaji Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Bw. Locken Massawe, alitoa shukurani zake kwa Serikali kwa kuonesha umuhimu wa kuwakutanisha na kusikiliza maoni yao.

“Kwa sasa hivi tunaona tofauti kabisa na kule tulikotoka kwa sababu hata ukiangalia kwa sasa hivi muundo uliotumika wa kuchukua maoni ni ile staili inayokufanya wewe mwenyewe unapata imani kwamba linalokwenda mbele ya Serikali litafanyiwa kazi na serikali imelipa kipaumbele” alisistiza Bw. Massawe.
Mfanyabiashara kutoka Kampuni ya Xin Si Lu Bi. Suvi Zeng, akitoa maoni yake kuhusiana na sekta ya uvuvi wakati wa Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha.

Naye Mtunza Hazina wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Arusha, Bi. Ester Msule, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kupitia Wizara ya Fedha na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kwa kuwaletea Kongamano hilo lililowawezesha kutoa maoni yao wakiwa na imani kubwa kwamba, yatafanyiwa kazi kama walivyoyawasilisha na kuwaletea mabadiliko katika biashara zao na kulipa kodi stahiki kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria Kongamano la Kodi wakisikiliza maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara mbalimbali waliohudhuria katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha.

“Naishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na TCCIA kuleta Kongamano kama hili na tunapata fursa ya kuja kujieleza sisi kama wakulima na wafanyabiashara kwa ujumla kwa sababu sisi viongozi nyuma yetu kuna wafanyabiashara wakubwa kwa hiyo tumemshukuru sana Mhe. Rais pia kutuletea Kongamano kama hili na tumekuja tumejifunza mambo mengi sana; kwanza Mama ametuheshimisha kutusikiliza sisi Jumuiya ya Wafanyabiashara ili tuwawakilishe wenzetu wengine. Kwa hiyo tunashukuru Wizara ya Fedha imesikiliza kero zetu na tunajua watakwenda kuyafanyia kazi haya tuliyoyaeleza,”alisema Bi. Msule.

Aidha, Afisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Arusha, Bi. Sia Maruda, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutaka kuboresha mfumo wa kodi Tanzania lakini pia ameishukuru Wizara ya Fedha kwa kutembelea Mkoa wa Arusha ili kujua kero na changamoto za kodi zinazowakabili wafanyabiashara.
Picha ya pamoja na wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali, katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Arusha).

“Kupitia kongamano hili tunaamini “Finance Bill” inayokuja maboresho yaliyotolewa yatawasilishwa vizuri na wafanyabiashara wameweza kupata suluhisho. Tunachotaka sisi ni kujenga nchi yetu kwa pamoja, hatutaki kukweka kodi na wala hatushauri kukwepa kodi lakini tunataka kujenga mazingira ambayo mfanyabiashara atafanya biashara bila kuona kwamba anakandamizwa,”alisisitiza Bi. Marunda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news