Serikali kuendelea kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili kikanda na Kimataifa

DODOMA-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) ameliambia Bunge kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza na kutangaza Lugha ya Kiswahili duniani ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha matumizi ya Lugha hiyo katika Taasisi za Kikanda na Kimataifa na kuhakikisha inafundishwa kama taaluma ili kuzalisha wakalimani bora.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akizungumza wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni jijini Dodoma tarehe 1 Novemba 2024.

Mhe. Chumi ametoa kauli hiyo Bungeni, jijini Dodoma leo tarehe 01 Novemba 2024 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Hawa Subira Mwaifunga aliyetaka kujua kwa nini Lugha ya Kiswahili haitumiki kwenye Jukwaa la Wabunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF) kama inavyotumika kwenye Bunge la Afrika (PAP).

Mhe. Chumi ambaye alizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwenye nafasi hiyo, mwezi Julai 2024, amesema kuwa Tanzania imeendelea na jitihada mbalimbali za kukuza Lugha ya Kiswahili na kufanikisha Lugha hiyo kuridhiwa na SADC kama lugha ya kazi katika Mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali na Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo tangu mwaka 2019, huku ikiendelea na jitihada za kukiwezesha Kiswahili kutumika katika Mikutano ya ngazi ya Makatibu Wakuu na Taasisi nyingine za SADC ikiwemo Jukwaa la Wabunge la SADC.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Mwaifunga, kuhusu changamoto kwa Serikali katika kugharamia wakalimani ili kukitangaza Kiswahili, Mhe. Chumi amesema kwamba Serikali kupitia ushawishi wake, imefanikiwa kujenga hoja ya kushirikiana na SADC katika kugharamia wakalimali na hoja hiyo kukubalika ambapo sasa SADC inagharamia wakalimani katika mikutano yote inayoendelea chini ya Jumuiaya hiyo.

“Kuhusu wakalimani, ni kweli kuna gharama kubwa za kugharamia suala zima la ukalimani. Hata hivyo, kwa ushawishi Serikali imefanikiwa kujenga hoja ili kusudi mzigo huo uweze kubebwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na SADC na kwa sasa SADC katika mikutano inayoendelea wamekubali kugharamia wakalimani,” alisema Mhe. Chumi.

Kadhalika ameongeza kusema, ili lugha iwe rasmi yapo mabadiliko ya kanuni na miongozo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ndani ya SADC na kwamba Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kipengele hicho kinafanyiwa marekebisho ili kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika Jumuiya ya SADC.
Mhe, Chumi akijibu swali Bungeni

Aidha, akijibu swali la nyongeza la Mhe. Anatropia Lwehikila kuhusu mikakati ya Serikali katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa wakalimani kutoka Tanzania, Mhe. Chumi amesema kuwa, ukalimani ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine na kutoa wito kwa wadau mbalimbali vikiwemo Vyuo chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwekeza katika kuhakikisha mafunzo ya ukalimani yanatolewa kama taaluma ili kuwawezesha wakalimani kutoka Tanzania kukidhi vigezo vinavyotakiwa na kutumiwa katika mikutano mbalimbali duniani.

‘Ukalimani ni taaluma, kujua Kiswahili na Kiingereza kama lugha haitoshi kukufanya kuwa mkalimani. Hivyo, natoa wito kwa Vyuo vyetu nchini chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha wanatoa mafunzo ya ukalimani kama taaluma ili na sisi tunapokwenda katika mikutano mbalimbali duniani tukutane na wakalimani ambao ni watanzania’ alisisitiza Mhe. Chumi.

Kadhalika amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) na Balozi za Tanzania imeendelea na jitihada za kutangaza Kiswahili kama bidhaa kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa ikiwemo makongamano, mikutano pamoja na kuwa na madawati ya kiswahili kwenye Balozi za Tanzania na kuzishawishi Balozi zinazowakilisha nchi zao hapa Tanzania kuwa na madawati ya namna hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news