Serikali yaanza kuwasaka waliohusika ukatili wa kingono kwa mtoto, Waziri Pembe abainisha mengi

ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema, yeyote ambaye atabainika kuhusika na ukatili wa kingono kwa mtoto Khadija atachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Zanzibar,Mheshimiwa Riziki Pembe Juma ameyasema hayo leo Novemba 21,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Wizara uliopo Kinazini Mkoa wa Mjini Magharibi jijini Zanzibar.

Mheshimiwa Waziri Pembe alikuwa akizungumzia kuhusu Maadhimisho ya Siku 16 za Harakati za Kupinga Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia.

"Tukiwa tunaelekea kuadhimisha siku 16 za harakati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia napenda kutoa masikitiko yangu makubwa kwa kitendo cha ukatili alichofanyiwa mtoto Khadija mwenye umri wa miaka sita kudhalilishwa kingono na baadae kupoteza uhai wake.

"Wizara imesikitikitishwa na kitendo hicho na kwa kushirikiana na mamlaka nyingine haitosita kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kufanya ukatili na udhalilishaji huo."

Waziri Pembe amesema,chimbuko la siku 16 za wanaharakati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ni kampeni ya ulimwenguni kote ambapo chimbuko lake linatokana na mkutano wa wanaharakati dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia.
Amesema, mkutano huo ulifanyika mjini Bogota nchini Colombia huko Amerika ya Kati tarehe 18 hadi 21 Novemba 1991.

Amesema, mkutano huo ulijikita katika kubadilishana mawazo juu ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia duniani.

"Mkutano huo uliazimia na kuchagua siku 16 kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Disemba ambayo ni siku za kimataifa dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji na hadi tarehe 10 Disemba ambayo ni siku ya Kimataifa ya haki za binaadamu kwa lengo la kuhusisha masuala ya ukatili na masuala ya haki za binadamu."

Waziri Pembe amesema,mwaka 1999 Umoja wa Mataifa uliridhia na kutangaza kuwa siku 16 za wanaharakati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

"Kwa hapa kwetu Zanzibar harakati hizi zilianzia mwaka 2011 na kuendelea hadi leo kwa kufanya shughuli mbalimbali."

Amesema,lengo la maadhimisho hayo ni kutathmini juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na wadau katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, kuhamasisha wadau na jamii kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi na kupanga mikakati mipya ya kupambana na kadhia hiyo.
"Kwa kawaida maadhimisho haya kwa kila mwaka huwa na ujumbe maalum unaoakisi mikakati ya kuondoa tatizo hilo."

Waziri Pembe amesema,kwa mwaka huu wamelenga kuwaleta pamoja watu wote kwa kupaza sauti na kuonesha hisia zao na kila mmoja kuonesha hatua za kuchukua katika kukabiliana na tatizo la vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia.

Amesema,ujumbe wa mwaka huu wa 2024 ni "kuelekea 2030 tuungane kutafakari na kuchukua hatua kumaliza udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto Zanzibar."

"Kwa hakika kauli mbiu hii inatupa ari ya kukaa kwa pamoja na kushirikiana ana kwa ana kutokomeza kabisa vitendo vya Udhalilishaji wa Kijinsia ambao umekuwa tishio hapa Zanzibar na kuumiza akili za walio wengi."

Waziri Pembe amesema,kwa mwaka huu maadhimisho ya siku 16 yanatarajiwa kuzinduliwa Zanzibar na kufungwa kisiwani Pemba.

Amesema,katika siku hizi 16 za harakati za kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa shughuli mbalimbali zikiwemo kuanda shindano la uandishi wa Insha kwa wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu kuhusiana na vitendo vya udhalilishaji kwa Wanafunzi.

"Shuguli nyingine ambazo zinatarajiwa kufanywa na Wizara ni Kongamano la Wajasiriliamali wanawake na Wanaharakati wengine Unguja na Pemba kuhusiana na mapambano dhidi ya ukatili pamoja na kupewa elimu ya ujasiriamali ikiwemo uandaaji wa miradi.
"Kufanya mikutano na wadau wa GBV na waratibu wa wanawake na watoto wa shehia pamoja na kutoa mafunzo kwa Wanafunzi kupitia Serikali zao za wanafunzi katika Skuli.

"Wizara pia imepanga kuwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya kupinga udhalilishaji na ukatili dhidi ya wazee, wanawake na watoto wakiwemo Tamwa, Zafela, Mahakama, Fawe, Dawati la jinsia pamoja na wadau wengine kwa kuwasilisha shughuli zinazotekelezwa na taasisi zao na kutoa elimu kwa wananchi watakaofika katika ufunguzi huo."

Katika hatua nyingine,Waziri Pembe amesema,jumla ya matukio 165 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwezi wa Julai 2024,ambapo waathirika walikuwa 165 ikiwa waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 86.1.

Aidha,wanawake asilimia 10.9 na wanaume asilimia 3.0.Miongoni mwa watoto ambao wameathirika ni 142, wasichana walikuwa 115 sawa na asilimia 1.0 na wavulana walikuwa 27 sawa na asilimia 19.0.

"Matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yaliyoriptiwa kwa mwezi Agosti 2024 yalikuwa ni 157 ambapo waathirika wengi walikuwa ni watoto sawa na asilimia 87.2 wanawake asilimia 11.5 na wanaume asilimia 1.3.

"Miongoni mwa waathirika watoto ni 137, wasichana walikuwa 112 sawa na asilimia 81.8 na wavulana walikuwa 25 sawa na asilimia 18.2."

Waziri Pembe amesema,mwezi Septemba,2024 jumla ya matukio 148 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa ambapo waathirika walikuwa 148.

Amesema,waathirika wengi walikuwa watoto kuanzia kuzaliwa hadi miaka 17 sawa na asilimia 87.9, wanawake miaka 18 na zaidi sawa na asilimia 7.4 na wanaume kuanzia miaka 18 na kuendelea sawa na asilimia 4.7.

"Miongoni mwa watoto waathirika 130 Wasichana walikuwa 107 sawa na asilimia 82.3 na wavulana walikuwa 23 sawa na asilimia 17.7."

Waziri Pembe amesema,takwimu hizo zinaonesha kupungua kidogo kwa matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ukilinganisha na mwezi Julai na hii ni kwa mujibu wa toleo la Takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar.

"Hii haimaanishi tupunguze kasi ya kupambana na vitendo hivyo bali nguvu zinahitajika zaidi ili tuweze kuyatokomeza kabisa matendo hayo thakili."

Amesema, pamoja na juhudi nyingi zinazochukuliwa na Serikali na zisizo za Kiserikali, bado vitendo vya udhalilishaji vinaendelea.

"Jamii bado haijashajiika na kufahamu athari ya vitendo hivi na badala yake inaendeleza rushwa muhali.

"Hivyo, ni jukumu letu sote kuendeleza kutoa taaluma ya athari za vitendo hivi ili jamii ipate uelewa wa kina kuhusiana na ubaya wa vitendo hivyo."

Pia, Waziri Pembe amelishukuru Jeshi la Polisi, vyombo vya habari na mashirika ambayo wamekuwa wakishirikiana pamoja katika harakati hizo ambayo ni Shirika la UNWOMEN, UNFPA Tanzania, UNICEF, IOM, UNESCO,

Save the Children, Zanzibar Maisha Bora Foundation, PATHFINDER, C-SEMA, ACTIONAID, Asma Mwinyi Foundation, TAMWA, ZAFELA, ZCRF na mengineo.

"Mashirika haya yamekuwa yakituunga mkono kwenye mapambano ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news