Serikali yachukua hatua za haraka kuokoa waliofukiwa na kifusi ajali ya kuporomoka jengo la ghorofa Kariakoo

DAR-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na juhudi kubwa za uokoaji baada ya ghorofa mbili kuanguka eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, tukio lililotokea jana na kusababisha maafa na huzuni kwa Watanzania wengi.
Katika kujali maisha ya wananchi wake, serikali imeonyesha mshikamano wa hali ya juu kwa kushirikisha vikosi vyote muhimu katika operesheni ya uokoaji.

Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, pamoja na wataalamu wa usaidizi wa dharura wapo eneo la tukio wakifanya kazi usiku na mchana kuokoa maisha ya watu waliokwama chini ya vifusi.

Serikali pia imepeleka vifaa maalum vya kisasa, ikiwemo mitungi ya gesi ya hewa ya oxgeni kwa ajili ya kupumua kwa watakaokuwa na hali mbaya, magari ya kuchimba (excavators), malori ya kubeba kifusi na vifaa vingine vya uokoaji.

Katika kuhakikisha waliojeruhiwa wanapata huduma bora, magari ya wagonjwa (ambulance) yamekita kambi eneo hilo kwa ajili ya kuwahisha majeruhi hospitalini.

Pia, wananchi wameombwa kushirikiana kwa kutoa taarifa za ndugu au jamaa waliokuwa karibu na eneo la tukio ili kurahisisha juhudi za uokoaji.

Kwa mara nyingine, Serikali inatoa pole nyingi kwa wale waliopoteza wapendwa wao kwenye tukio hili na kuwahakikishia kuwa hatua zote zinazochukuliwa zina lengo la kuokoa maisha na kupunguza madhara. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema:

Nimesikitika kupokea taarifa ya ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.

"Nimeuagiza Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha zoezi la uokoaji na tiba kwa majeruhi."

Wakati hilo likiendelea na tukimuomba Mwenyezi Mungu awape pona ya haraka majeruhi, tuwaombee pia utulivu na subra ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wenzetu wanaotafuta riziki zao katika eneo hili muhimu kibiashara nchini ambao kwa namna mbalimbali wameathiriwa na ajali hii"

Pia Mheshimiwa Rais amesema: "Hivi punde nimezungumza kwa kirefu na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mbunge) kuhusiana na ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, na kazi ya uokoaji inayoendelea.

"Nimempa maelekezo kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa haraka na ufanisi, na niendelee kupata taarifa ya kila hatua ya maendeleo yake."

Hili ni wakati wa Watanzania kushikamana na kuwapa msaada wa kihisia waathirika wa tukio hili. Kila mkono wa msaada, sala, na moyo wa faraja unahitajika ili kulivusha taifa hili kwenye kipindi hiki kigumu.

Serikali inaomba uvumilivu na ushirikiano wa wananchi wote wakati juhudi za uokoaji zikiendelea kwa kasi. Amani, mshikamano, na upendo vitatusaidia kushinda changamoto hii pamoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news