NA EVA NGOWI
WF
SERIKALI ina jukumu kubwa la kuweka mikakati ya kuendelea kurasimisha biashara nchini na kuhamasisha utumiaji wa mashine za kielektroniki katika utoaji wa risiti ikiwa ni pamoja na kutumia risiti hizo kujipatia zawadi kupitia Tuzo ya Uzalendo inayotarajiwa kufunguliwa rasmi hivi punde.
Picha ya pamoja ya wadau mbalimbali katika sekta ya uvuvi, kilimo, ufugaji, wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo waliohudhuria katika Kongamano la Kodi lililofanyika Kanda ya Ziwa Kigoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Kigoma).
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama, wakati wa Kongamano la Kodi lililofanyika Mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama, akitoa ufafanuzi wakati wa Kongamano la Kodi kwa wadau mbalimbali (hawamo pichani) lililofanyika katika Kanda ya Ziwa (Kigoma).
Bw. Manyama alisema, maoni mbalimbali yanayotolewa katika Makongamano hayo ya Kodi yatasaidia kuibua vyanzo vipya vya mapato na kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje pamoja na kuendelea kubainisha maeneo yenye changamoto zaidi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama (Katikati) akitoa ufafanuzi kwa wavuvi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali (hawamo pichani) walioshiriki katika Kongamano la Kodi kulia kwake ni Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo- TCCIA Mkoa wa Kigoma Bw. Obadi Kabuga na kushoto kwake ni Katibu Tawala Msaidizi- Viwanda, Biashara na Uwekezaji Kigoma Bw. Deogratias Sangu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo - TCCIA Mkoa wa Kigoma, Bw. Obadi Kabuga, alisema kuwa Kongamano hilo la Kodi limekuwa funzo na litasaidia Serikali kufanya biashara kwa kushirikiana na nchi zinazoizunguka, kwani sera zilizopo zinakinzana na sera za nchi jirani na kuiomba Serikali kufanya utafiti wa sera zake kabla ya kupeleka maboresho ya sera katika Bunge lijalo 2025/2026.
Meneja wa Maendeleo ya Biashara, Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania - TCCIA Bw. Mercy Philipo akiwasilisha mada (haionekani pichani) kuhusiana na maoni yaliyofanyiwa kazi katika Makongamano ya Kodi Kikanda yaliyofanyika mwaka jana (2023) Kanda ya Ziwa Kigoma.
“Tunaomba mabadiliko ya Sera yatakapopelekwa Bungeni yafanyiwe utafiti kabla ya kufanya mabadiliko, wenzetu wana sera gani, ili zitakapokuja zile sera jumuishi ambazo zitakuwa na mfanano zitaleta uchumi mzuri na hususan katika Mkoa wetu wa Kigoma pamoja na Tanzania nzima” Alifafanua Bw. Kabuga.
Katibu wa Chemba ya Biashara ya Wanawake Kigoma- TWCC, Bi. Chichi Kamandwa akitoa maoni yake kuhusiana na kodi ya mabango ya matangazo ya biashara wakati wa Kongamano la Kodi lililofanyika Kanda ya Ziwa Kigoma.
Bw. Kabuga alihitimisha kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiamini TCCIA pamoja na Wizara ya Fedha kwa pamoja kuandaa Makongamano hayo ya Kodi Kikanda, ambapo mwitikio kwa wanakigoma ulikuwa mkubwa na wameitumia fursa hiyo vizuri kwa kutoa maoni na changamoto mbalimbali.
Meneja Mwandamizi wa Kiwanda cha Uzalishaji Chumvi - Uvinza, Bw. Venkataraman Lyappan, akitoa maoni yake kuhusiana na sekta ya viwanda upande wa uzalishaji Chumvi, katika Kongamano la Kodi Kanda ya Ziwa Kigoma.
Kongamano hili la Kodi bado liko kwenye Kanda ya Ziwa (Kigoma),Makongamano haya ya Kikanda yalianzia Kanda ya Kati Dodoma, Kanda ya Kaskazini Arusha na yanaendelea katika Kanda nyingine