DODOMA-Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda tarehe 23, Novemba, 2024 amefungua Mafunzo elekezi kwa maafisa Uthibiti ubora wa shule wa wilaya yatakayochukua siku tatu jijini Dodoma.
Serikali imechukua hatua kubwa ya kuimarisha elimu kwa kutoa kibali cha kuajiri walimu 4,000 wa somo la biashara. Walimu hawa watafundisha wanafunzi wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, wakilenga kuwapa maarifa muhimu kupitia mtaala mpya unaolenga kuleta mapinduzi ya elimu nchini.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kufungua Mafunzo Elekezi kwa Maafisa Uthibiti Ubora wa Wilaya Wateule amesema hatua hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi msingi thabiti wa maarifa ya biashara.
“Tunataka wanafunzi wote wa sekondari wapate maarifa ya biashara, lengo ni kuwaandaa watoto wetu kujitegemea na kufanya maamuzi bora baada ya kumaliza shule,”amesema Mkenda.
Amewataka wathibiti ubora hao kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri na walimu ili kuimarisha mtandao wa mawasiliano utakaowezesha kutambua na kutatua changamoto kwa haraka.