DAR-Kupitia ushindi wa mabao 4-0 ambao Simba SC wameupata dhidi ya KMC FC umewafanya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Mtanange huo umepigwa Novemba 6,2024 katika Dimba la KMC Complex lililopo Mwenge katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Awesu Awesu ambaye ni kiungo mshambuliaji aliwapatia bao la kwanza dakika ya 25 kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi ya Steven Mukwala.
Naye Jean Charles Ahoua aliwapatia bao la pili kwa mkwaju wa penati dakika ya 36 baada ya mlinzi Shomari Kapombe kufanyiwa madhambi ndani ya 18.
Edwin Balua aliwapatia bao la tatu dakika ya 66 kwa shuti kali ndani ya 18 lilomshinda mlinda mlango wa KMC, Fabien Mutombora baada ya kupokea pasi kutoka kwa Valentine Nouma.
Aidha,dakika mbili baadae Ahoua alitufungia bao la nne baada ya Kutumia vizuri makosa ya Mlinzi wa KMC, Ismail Gambo.
Kocha Fadlu Davids alifanya mabadiliko ya kuwatoa Awesu Awesu, Debora Fernandes, Ladaki Chasambi, Karaboue Chamou na Fabrice Ngoma kuwaingiza Omary Omary, Mzamiru Yassin, Edwin Balua, Kibu Denis na Hussein Kazi.
Katika mchezo huo Jean Charles Ahoua amechaguliwa nyota bora wa mchezo baada ya kuhusika kwenye mabao mawili pamoja na kuonyesha kiwango safi.
Ushindi huu umewafanya kufikisha alama 25 baada ya kucheza mechi 10 wakipaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo yenye msisimko wa kipekee.
Wakati huo huo, Kocha Fadlu Davids amefanya mabadiliko ya wachezaji watano ukilinganisha na kikosi kilichocheza mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa FC.
Kocha Fadlu aliwaanzisha Valentine Nouma, Debora Fernandes, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua na Awesu Awesu wakichukua nafasi za Mohamed Hussein, Augustine Okajepha, Leonel Ateba, Joshua Mutale na Kibu Denis.
Hiki hapa kikosi kamili kilichopangwa:
Moussa Camara (26), Shomari Kapombe (12), Valentine Nouma (29), Karaboue Chamou (2), Che Malone (20), Fabrice Ngoma (6), Ladaki Chasambi (36), Debora Fernandes (17), Steven Mukwala (11), Jean Charles Ahoua (10), Awesu Awesu (23).
Wachezaji wa Akiba:
Ally Salim (1), Mohamed Hussein (15), Hussein Kazi (4), Augustine Okajepha (25), Omary Omary (8), Mzamiru Yassin (19), Kibu Denis (38), Edwin Balua (37), Benjamin William (50), Shedrack Daniel (52).