DAR-Tabora United FC imewashushia kipigo cha mabao 3-1 Young Africans Sports Club, matokeo ambayo yamesababisha majonzi makubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Ni kupitia mtanange wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambao umepigwa Novemba 7,2024 katika Dimba la Azam Complex lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Young Africans Sports Club ambao ni mabingwa wa ligi hiyo wamepoteza mchezo wa pili mfululizo.
Offen Francis Chikola dakika ya 19 ndiye aliyefungua pazia la mabao baada ya kuwapa waajiri wake Tabora United FC bao la kwanza.
Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 45' ndipo akagonga msumari mwingine ambao ulionekana kuwatia majozi wana Yanga.
Katika kipindi cha pili, Tabora United FC walirejea na shauku ya kupata matokeo zaidi ambapo dakika ya 77,Nelson Omba Munganga akimalizia pasi ya mshambuliaji Ibrahim Ahmada alifunga bao la 3.
Young Africans Sports Club wakiwa katika kipindi kigumu,Clement Francis Mzize dakika ya 90' akimalizia pasi ya mshambuliaji Prince Dube Mpumelelo aliwafuta machozi kwa bao moja.
Aidha,kwa kipigo hicho, Yanga SC wanasalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama 24.
Ni baada ya mechi 10 huku Tabora United wakisalia nafasi ya sita kwa alama 17 baada ya mechi 11 ambapo vinara kileleni ni Simba SC wenye alama 25 baada ya mechi 10.