ARUSHA-Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imefanya ufuatiliaji wa raslimali za umma katika utekelezaji wa miradi 28 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 32.15.
Ngailo amesema, miradi hiyo iliyofuatiliwa ni katika Sekta ya Ujenzi, Miundombinu, Maji, Afya na Elimu.
Amesema,baada ya kufanya ufuatiliaji TAKUKURU ilitoa jumla ya mapendekezo 63 kwa mamlaka na taasisi zinazotekeleza miradi husika kwa lengo la kuziba mianya ya rushwa iliyobainika kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.
Pia, amesema TAKUKURU Mkoa wa Arusha ilifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na hadi kufikia Septemba, 2024 jumla ya mapendekezo 36 yalikuwa yametekelezwa.
"Aidha, TAKUKURU inaendelea na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo yaliyobakia ili kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa kwenye Mkoa wa Arusha inakuwa na thamani ya fedha,kuepusha uvujaji wa fedha za miradi.
"Na kuhakiksiha ushirikishwaji wa wananchi na kuepusha ucheleweshaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo."
Wakati huo huo, katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2024 TAKUKURU Mkoa wa Arusha imeendelea na jukumu la uchambuzi wa mifumo ya umma na binafsi.
Ngailo amesema,lengo ni kubaini mianya ya rushwa iliyopo kwenye mifumo hiyo na kushauri namna bora ya kuziba mianya ya rushwa kwa mujibu wa kifungu cha 7(A) & (C) cha PCCA [RE: 2022].
"Katika kipindi tajwa ofisi imefanya jumla ya chambuzi nne za mifumo.Aidha,zimefanyika warsha mbili na wadau kwa ajili ya kuwekeana maazimio ya kuziba mianya ya rushwa.
"Hivyo TAKUKURU inaendelea na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maazimio yaliyowekwa kwenye vikao vya warsha na wadau kwa ajili ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika."
Pia, Ngailo amesema Programu Rafiki ya TAKUKURU imetekelezwa katika kata 13 ambapo jumla ya kero 49 ziliibuliwa.
Amesema,wananchi kwa kushirikiana na TAKUKURU pamoja na viongozi kutoka taasisi ambazo kero hizo zinatokea walikaa kwa pamoja na kutatua baadhi ya kero hizo.
"Jumla ya kero 25 zilitatuliwa na kero 24 zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi.Kazi hii ikikamilika, ofisi au taasisi husika kwa kushirikiana na TAKUKURU watakutana na wananchi ili waweze kuwapa mrejesho."
Kwa upande wa Elimu kwa Umma,Ngailo amesema wamefanya semina 47, uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa 58, mikutano ya hadhara 41, naonesho tisa,nakala saba na vipindi vya redio saba.
Tags
Habari
Miradi ya Maendeleo
Programu Rafiki ya TAKUKURU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)