ARUSHA-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imesema, katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2024 iliendelea kupokea malalamiko kwa njia mbalimbali.
Katika kipindi tajwa jumla ya malalamiko 80 yalipokelewa ambapo kati ya hayo,malalamiko 65 yalihusu rushwa na 15 hayakuhusu rushwa.Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Bi.Zawadi Ngailo.
"Malalamiko ambayo hayakuhusu rushwa walalamikaji walishauriwa na majalada yalifungwa.
"Kwa yale yaliyohusu rushwa yapo katika hatua mbalimbali za uchunguzi.Aidha katika kipindi tajwa jumla ya kesi 14 zilifunguliwa mahakamani ambapo kesi 11 zinaendelea mahakamani, kesi mbili zimeshinda."
Mbali na hayo amesema, Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Arusha imejipanga kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuelimisha makundi muhimu katika uchaguzi huo na kuwaasa kutokujihusisha na vitendo vya rushwa.
Ngailo amesema,makundi yanayolengwa ni wagombea wa nafasi mbalimbali,viongozi wa vyama vya siasa vitavyoshiriki uchaguzi, wanachama wa vyama vya siasa, wasimamizi wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla ambao ni wapiga kura.
"Uelimishaji huo utafanyika kupitia mikutano ya hadhara,semina na vipindi vya radio. Sanjari na uelimishaji huu, programu ya TAKUKURU Rafiki itatumika kuwafikia na kuwaelimisha wananchi wa ngazi ya kata ambao ni wadau muhimu katika uchaguzi."
Pia, Ngailo amesema ofisi itaendelea kupokea na kufanyia kazi malalamiko yote ya vitendo vya rushwa kwa lengo la kuziba mianya ya rushwa na kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaobainika.
Aidha, Ngailo amesema ofisi itaendelea na ufuatiliaj wa matumizi ya fedha za umma zinazoelekezwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo hususani miradi ya maendeleo katika ngazi ya kata,mitaa na vijiji ili kuhakikisha kuwa zinatumika kama ilivyokusudiwa.
"Nitumie nafasi hii kuwaasa wananchi wa Mkoa wa Arusha kujiandaa na kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu, na kuchagua viongozi waadilifu watakaoiwezesha Serikali kuwaletea wananchi maendeleo."
TAKUKURU Mkoa wa Arusha imewahakikishia wananchi kuwa ipo tayari kushirikiana na mwananchi yeyote mwenye nia thabiti ya kudhibiti vitendo vya rushwa.
Tags
Habari
Programu Rafiki ya TAKUKURU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania