ZANZIBAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali za SMZ na SMT, zimeandaa mpango wa kuongeza vituo vya uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia teknolojia ya nyuklia wenye thamani ya Euro milioni 59.
Amesema, kupitia mpango huo, Serikali hizo zimedhamiria kuviongezea uwezo vituo vya Ocean Road, Dar es Salaam, Bugando, Mwanza na kuanzisha vituo vipya vinne kwa hospitali za Benjamini Mkapa Dodoma, KCMC Moshi, Mnazi Mmoja Zanzibar na Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, alipofungua Ofisi na Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kwa Zanzibar, huko Dunga Zuze, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema, kukamilika kwa mpango huo kutaongeza huduma za matibabu ya saratani kwa kutumia teknolojia ya nyuklia na Tanzania itakuwa na vituo sita vya Serikali katika kanda zote muhimu nchini.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza ujenzi wa Ofisi na Maabara hiyo ni chachu ya kuanza kwa ujenzi wa banki kwa ajili ya kuwekea vifaa vya nyuklia kwa hospitali za Benjamini Mkapa Dodoma na KCMC Moshi.
Vilevile Dk.Mwinyi ameeleza kwa maendeleo ya kiteknolojia ya nishati ya nyuklia pia yana uwezo wa kuchukua nafasi muhimu katika mchakato wa kuhama kuelekea mfumo wa nishati usio na kaboni (Carbon) au hewa ukaa yanayoweza kuzalisha umeme unaohitajika.
Halikadhalika , Dk. Mwinyi amezisisitiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana pamoja na Wizara ya Nishati na wadau wengine kuandaa mpango thabiti ili kuhakikisha Tanzania inaanza kunufaika na umeme wa nyuklia.