Tanzania ipo katika hatua nzuri kufanikisha mfumo wa Jamii Namba-Dkt.Mwasaga

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya TEHAMA Tanzania (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema,Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache duniani ambayo yapo katika hatua nzuri kufanikisha mfumo wa Jamii Namba.
Dkt.Mwasaga ameyasema hayo Novemba 14,2024 wakati wa mahojiano katika Kipindi cha Kasri la Kikeke kinachorushwa na Crown FM jijini Dar es Salaam.

Mfumo wa Jamii Namba ni utambulisho wa kipekee unaotolewa kwa kila mwananchi, ambao unaweza kutumika katika mifumo mbalimbali ya Serikali na hata sekta binafsi.

"Sasa, Afrika ina nchi nyingi zipo zaidi ya 54, kuna kikao kilifanyika miezi miwili iliyopita nchini Misri kuangalia nchi gani ambazo zimepiga hatua katika kujiandaa kuweza kutumia hizo namba za namna hiyo.

"Na katika ripoti iliyotoka Tanzania ipo katika nchi chache za Dunia ambazo tumepiga hatua kuwa na mfumo ambao upo tayari."

Dkt.Mwasaga amesema kuwa, hapa nchini tayari mfumo unaozungumza upo na mfumo kwa ajili ya kufanya malipo ya hapo kwa hapo na wenyewe upo.
"Kilichobaki sasa ni kufanya mifumo hiyo iweze kufanya kazi kwa pamoja, watu wapewe elimu ianze kutumika."

Amesema, katika kuziwezesha namba hizo kufanya kazi hadi nje ya nchi kuna Mfumo Wezeshi wa Kuwezesha Kutumia Namba nchi Nyingine.

"Sasa, hiyo inahitaji nchi za Afrika zikae pamoja, nchi zingine unakuta zimeshakubaliana baina ya nchi mbili mbili."

Jamii Namba hutumika kusimamia rekodi mbalimbali ikiwemo sekta za afya, elimu, uchumi na nyinginezo.

Agosti 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan alisisitiza umuhimu wa Jamii Namba ili kumaliza utitiri wa utambulisho wa namba zinazotumika sasa na kuwezesha mifumo kusomana nchini.

Dkt.Mwasaga anasema, Mfumo wa Jamii Namba ulivyotengenezwa nia yake ni kuondoa changamoto ya mtu kubeba rundo la vitambulisho.

"Watu wana vitambulisho vingi kwa sababu binadamu kazi anazofanya kila siku zinahitaji utambulisho.

"Ndiyo maana ukienda benki fulani wanakupa kitambulisho, ukienda shule hivyo hivyo unahitaji kitambulisho.
"Lakini, katika dunia ya kidijitali ya leo inatakiwa mtu aweze kutambulika mara moja na namba moja.

"Hao wengine wanataka kukutambua watatumia hiyo namba kupata taarifa zako wanazohitaji kupata na ndio duniani kote wanafanya hivyo.

"Sasa hili kuhakikisha hilo jambo linafanikiwa, kuna miundombinu ya kisasa, hiyo inaitwa miundombinu ya kidijitali ya umma."

Dkt.Mwasaga amesema, hiyo miundombinu ndiyo inawezesha kuondoa mzigo wa kutembea na mizigo mingi ambayo unatakiwa uzingatie vitu vitatu ambavyo vinamgusa mwananchi yeyote.

"Cha kwanza,wananchi wawe na namba moja ya kidijitali, cha pili mwananchi aweze kufanya miamala kwa kutumia mifumo ya kidijitali (digital payment).

"Cha tatu, mifumo iweze kuzungumza. Sasa, hivyo vitu vyote uweze kuvifanya na viweze kufanikiwa, Kwanza inatakiwa watu wapewe hiyo namba ya kidijitali."

Amesema, sababu ya kupewa namba hiyo ya kidijitali inatokana na mtu anapoamka asubuhi mpaka jioni anapitia mifumo mbalimbali ili kufanikisha shughuli zake za siku.

"Sasa hali ilivyo sasa hivi ni kwamba kwa mfano unatumia tuseme mifumo 20 katika kufanya kazi zako za kawaida, malipo na vitu vingine."Utakuta kila mfumo una namba yake inakutambua wewe, halafu hizo namba zifanane.

"Sasa, kukufanya wewe uweze au taarifa zako ziweze kupita katika mifumo mbalimbali bila shida, ni vizuri ukiwa na namba moja ya kidijitali.

"Hiyo namba inaweza kutumika sehemu zote,kwa hiyo unapata taarifa zako kama unataka kufungua akaunti, kama unaweza kutumia kwenye LUKU au kama unataka kwenda kujisajili sehemu yoyote."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news