BEIJING-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo katika mazungumzo ya utekelezaji wa maeneo 10 ya ushirikiano kati ya China na Afrika, Tanzania ikiwemo kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China katika Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba 2024 jijini Beijing, China.
Hayo yamebainishwa katika kikao kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel W. Shelukindo na Bw. Du Xiaohui, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China na Katibu Mkuu wa Kamati ya Ufuatiliaji ya China ya FOCAC kilichofanyika tarehe 11 Novemba 2024 jijini Dar es Salaam.
Halikadhalika, wawili hao walijadili kuhusu ufufuaji wa reli TAZARA na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa Tanzania na Zambia kwa kukuza uwekezaji na kuongeza biashara kati ya Tanzania na China.
Katika hatua nyingine, Balozi Du alieleza kuwa Serikali ya China inaunga mkono Programu ya Nishati Safi ya Kupikia na kuwa Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza programu hiyo ili Watanzania waweze kufaidika nayo.
Vilevile, alieleza kuwa Serikali ya China imeshaidhinisha utekelezaji wa mradi wa Ujenzi na Upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kuwa utekelezaji wake upo mbioni kuanza.
Kwa upande wake, Balozi Dkt. Shelukindo aliishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na alipongeza hatua ya China ya kuruhusu asilimia 100 ya bidhaa zote zinazotoka Tanzania kuingia katika soko la China bila kutozwa ushuru.
Mwisho, Balozi Dkt. Shelukindo na Balozi Du waliupongeza uhusiano wa kidiplomasia wa Tanzania na China kwa kufikisha miaka 60 mwaka huu 2024.