TCCIA yaipongeza Serikali kwa kuwashirikisha uboreshaji mifumo ya kodi

NA EVA NGOWI
WF Mwanza

CHEMBA ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) imeipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuandaa Makongamano ya Kikanda ya kukusanya maoni kutoka katika sekta mbalimbali ili kuboresha sera za kodi.
Kamishna Msaidizi Idara ya Sera Bw. William Mhoja (kulia) akiandika maoni yaliyokuwa yakitolewa na wafanyabiashara na wajasiriamali wa sekta mbalimbali katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Mwanza, kushoto ni Makamu wa Rais TCCIA- Biashara, Bw. Boniface Ndengo, akisikiliza maoni ya wafanyabiashara (hawamo pichani).

Hayo yalibainishwa na Makamu wa Rais TCCIA- (Biashara), Bw. Boniface Ndengo, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi lililofanyika jijini Mwanza.

Bw. Ndengo alisema kuwa kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, ina rasilimali kubwa hasa Ziwa Viktoria ambalo linaweza likatumika kama moja ya eneo ambalo linaweza kusaidia kuongeza uchumi kwa Kanda ya Ziwa na Taifa kwa jumla, kwa kurasimisha shughuli za sekta binafsi hasa wajasiriamali wadogo na kwa zile biashara mpya ili kupanua wigo wa kodi.
Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Mathias Kadebe akiwasilisha mada (hainekani pichani) kuhusiana na maoni yaliyofanyiwa kazi katika makongamano ya kodi kikanda yaliyofanyika mwaka jana (2023), jijini Mwanza.

“Serikali inaweza ikaona namna ya kurasimisha shughuli za sekta binafsi hasa wale wajasiriamali wadogo, biashara mpya ili kupanua wigo wa kodi lakini pia tumepokea maoni namna ambavyo rasilimali za nchi hasa Ziwa Viktoria linaweza likatumika kama moja ya maeneo ambayo yanaweza kusaidia kuongeza uchumi kwa eneo hili la Kanda ya Ziwa lakini uchumi wa Taifa kwa jumla,”amesisitiza Bw. Ndengo.
Mwakilishi wa Kampuni ya Furaha Nyanza Co. Ltd Bw. Baricat Khan, akitoa maoni kuhusiana na sekta ya viwanda jijini Mwanza.

Kwa upande wa Kamishna Msaidizi Idara ya Sera Bw. William Mhoja, alisema maoni yaliyotolewa na Jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Mwanza pamoja na sekta mbalimbali zilizohudhuria ni ya kujenga na yatasaidia sana kuboresha Sera za Kodi.

Bw. Mhoja alisema kuwa Serikali inaendelea kuweka na kutekeleza mikakati mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa inaboresha usimamizi wa kodi, ada na tozo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuibua vyanzo vipya ili kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa kibajeti na kuhakikisha upatikanaji na usalama wa chakula.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mwanza na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wauza Samaki Mwaloni L.T.D (USAMWA) Soko la Kirumba Mwaloni Bw. Erasto Balosha akichangia maoni yake kuhusiana na sekta ya uvuvi katika kongamano la kodi kikanda lililofanyika jijini Mwanza.

Naye Mwenyekiti wa TCCIA- Mwanza Bw. Gabriel Chacha aliipongeza Serikali namna ambavyo imeweza kufanyia kazi maoni yaliyotolewa hasa kwa wakulima kwa kupunguziwa kodi kwenye matrekta na mazao ya nyuki.

“Kwa namna hii Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kupitia Wizara ya Fedha, naipongeza kwa namna ambavyo imetengeneza huu utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara imewasogeza karibu na Serikali na kujenga mahusiano mazuri na kujenga kuaminiana,” Alisema Bw. Chacha.
Picha ya pamoja ya Kamati ya ukusanyaji wa maoni katika Kongamano la Kodi lililofanyika Kikanda, jijini Mwanza.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mwanza).

Kwa sasa Kongamano hili la Kodi liko kwenye Kanda ya Ziwa (Mwanza), yalianzia Kanda ya Kati Dodoma, na Kanda ya Kaskazini-Arusha na yataendelea katika Kanda nyingine, yakishirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali ziliwemo Sekta za Uvuvi, Umeme Jua (Solar), Usafirishaji, Mahoteli, Habari, Elimu (Shule binafsi), Viumbe Maji, Mifugo, Madini, Sekta ya Matukio, Viwanda vya dawa ya binadamu, Jumuiya ya Wafanyabiasha Tanzania Mkoa wa Mwanza, Shirikisho la umoja wa Machinga Tanzania-SHIUMA, Taasisi za Dini na Ujenzi na Masoko ya Samaki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news