DODOMA-Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC),Dkt. Benson Ndiege amesema Tume imedhamiria kushirikiana na Wadau kukuza na kuendeleza Ushirika ili uweze kuendeshwa Kibiashara kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa Vyama vya Ushirika.
Mrajis amesema hayo wakati wa utiaji saini wa Randama ya Makubaliano (MoU) kati ya Tume na Chuo cha Biashara (CBE) Novemba 20, 2024 jijini Dodoma.
Akiongea katika kikao hicho Mrajis amebainisha kuwa kwa sasa moja ya Vipaumbele vya Tume ni pamoja na kuhakikisha kuwa Ushirika unajiendesha kibiashara ili kutoa faida na kuongeza manufaa kiuchumi kwa Wanaushirika na wadau wengine.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Biashara, Prof. Edda Lwoga amesema, CBE iko tayari kushirikiana na Tume katika kufanya Tafiti mbalimbali za kutatua changamoto za Ushirika, kutoa mafunzo yatakayosaidia kuendesha vyama kibiashara pamoja na kutoa Ushauri wa Kitaalamu.
Pamoja na mambo mengine, TCDC na CBE pia zitashirikiana katika kuwapa fursa wanafunzi wa CBE kujifunza kwa vitendo ili kupata uzoefu wa kimasomo pamoja na kuchangia ujuzi katika kuongeza tija ya uendeshaji wa Vyama vya Ushirika.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Tume pamoja na Chuo cha Biashara.