TABORA-Watu 14 wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa katika ajali ya gari aina ya Toyota Hiace lenye usajili namba T 562 DGG.
Ni baada ya dereva wa gari hilo ambaye hajafahamika jina, kugonga fuso Mitsubishi lenye usajili namba T 361 CSB katika Kijiji cha Mwansengo katika Kata ya Itobo wilayani Nzega mkoani Tabora.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema, waliofariki katika ajali hiyo ni wanaume wanane, wanawake wanne na watoto wawili huku majeruhi wakiwa ni tisa.
“Novemba 7,2024 majira ya saa mbili na dakika ishirini kuna ajali imetokea katika barabara ya Itobo-Bukene katika Kijiji cha Mwansengo, Kata ya Itobo ambapo dereva wa gari lenye namba za usajili T. 562 DGG Toyota Haice likiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina alikimbia.
"Baada ya kugonga gari namba T. 361 CSB, Mitsubishi Fuso na kusababisha vifo vya watu 14 na chanzo cha ajali hii ni uzembe wa dereva ambaye alikuwa akijaribu kulipita lori lililokuwa mbele yake na kushindwa kulimudu gari lake na kuligonga lori upande wa kulia kwa nyuma na kuingia chini ya uvungu wa lori.”
Kamanda huyo amesema,miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega na miili tisa imetambuliwa na ndugu.
Hata hivyo, ametoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto barabarani kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani.