NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania imesema kuwa, ili mtu au taasisi iweze kukidhi vigezo vya kupata leseni ya kuendesha biashara ya kutoa mikopo kupitia huduma ndogo za fedha Daraja la Pili inapaswa awe na mtaji kuanzia shilingi milioni 20 taslimu,kusajiliwa na kuwasilisha Sera ya Mkopo.
Meneja Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Bi. Mary Ngassa ameyasema hayo Novemba 14, 2024 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam katika mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari.
Ni kuhusu Watoa Huduma Ndogo za Fedha Daraja la Pili abao wanatoa huduma za mikopo kwa njia ya mtandao.
"Utamtambuaje kama huyu ni halali au ni feki? Kwa kuwa umeweza kuingia mtandaoni, tunashauri na tunaomba uingie kwenye mtandao wa Benki Kuu uweze kuangalia orodha ya wale ambao ni halali.
“Lakini, hata sisi hawa feki tutaanza kuchukua hatua kwenye mtandao, tutatuma kwenye mtandao tuseme kwamba hawa hapa, tumewapa leseni, lakini Apps hizi hatuzifahamu na hatuzitambui kwa hiyo tunashauri mkae mbali nazo.
"Kwa sababu, tumeona tukiendelea kubaki na hawa tu ambao tunawatambua, watu wanaingia kule kupata huduma na wakishapata tatizo ndiyo wanakuja Benki Kuu.
"Hivyo, tumeona bora tuzitangaze kule, lakini pia tutatoa taarifa kwa umma ya kuelezea kwamba, hawa na hawa hawana kibali cha Benki Kuu, wapo mtandaoni, mwananchi tunawaomba msijihusishe nao.”
Katika hatua nyingine, Ngassa amesema mtaji kwa mtu au taasisi za huduma ndogo za fedha Daraja la Pili unaanzia shilingi milioni 20.
“Uwe nayo keshi, ukaingize benki utatuletea uthibitisho.Sisi tunasema, mtaji usipungue shilingi milioni 20, kiwango cha chini kabisa ni shilingi milioni 20, halafu wakati wa maombi tunahitaji kujua hiyo milioni 20 yake ameipata wapi, na uthibitisho wake kule ilikotokea.
“Kwa mfano wewe ni mwajiriwa ukasema mtaji ni milioni 20, utatuletea uthibitisho kwamba wewe ni mwajiriwa, ukihusisha mkataba wa kazi, salary slips zako za karibuni, na bank statement yako tuone hizo saving ulizotuambia.”
Kwa upande wa wakulima,Ngassa amesema watapaswa kupeleka Benki Kuu vithibitisho vyao kwamba huko alipo yeye ni mkulima na anatambulika.
“Na vyombo vya kule kijijini kwake, kama mkulima na hayo mauzo aliyouza mpaka kusave hiyo milioni 20.
“Kwa hiyo tunapokea sababu kadhaa, vyanzo vyake vya mtaji,lakini vyanzo hivyo anakuja navyo yeye hapa Benki Kuu na hatuna platform ya kuwapa mitaji hao watoa huduma ndogo ndogo za fedha daraja la pili.
"Kwa hiyo ni juhudi zake mwenyewe kujitafutia mtaji wake.Pia,atapaswa kuwasilisha Sera ya Mkopo ikionesha aina mbalimbali za mikopo unayotoa,muda, riba,ada, tozo,vigezo vyake.
"Lakini, pia utatuonesha wewe huko wapi, biashara hiyo utaifanyia wapi kwa maana ya eneo gani, wadhamini wako wasiopungua wawili.”
Ngassa amesema, pia kuna dodoso ambalo utajaza ambalo litakuwa linaonesha tabia, historia yako kama umeshawahi kushtakiwa mahali kokote na sababu.
“Lakini, pia utatuletea wadhamini wako wawili na watatuletea uthibitisho wa chanzo chako cha mtaji. Huo, mtaji wako wa shilingi milioni 20 utatuletea uthibitisho wako umeupataje,na utaapa kwamba hiyo njia uliyoipatia ni njia safi na salama.
“Kwa hiyo utaapa kwa mwanasheria kwamba ulipataje, kwa hiyo utatuletea huo uthibitisho baada ya hapo utaweka hiyo hela benki na utatuletea bank statement na utaandika barua kwa Gavana kuomba kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha na upewe leseni na Benki Kuu.”
Katika hatua nyingine Ngassa amesema, katika utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018,Benki Kuu imepata mapokeo chanya na mwamko katika kuzingatia sheria hiyo na kanuni.
Pia,wamefanikiwa kuimarisha mahusiano ya kikazi baina ya Benki Kuu na watoa huduma ikiwemo kupata mwamko mkubwa kwa watoa huduma ndogo za fedha katika kuwasilisha maombi ya leseni.
Vilevile, kuanzishwa kwa Sekta ya Kitaalam ya Huduma Ndogo za Fedha (Microfinance Certification Program).
Pia amesema, licha ya mafanikio kuna changamoto katika utekelezaji wa sheria hiyo hususani uelewa mdogo wa sheria na kanuni miongoni mwa watoa huduma na walaji.
Ameeleza kuwa,kufuatia changamoto ya ukiukwaji wa sheria katika utoaji wa mikopo kidijitali, Benki Kuu ilitoa Mwongozo kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali wa mwaka 2024, mwezi Agosti 2024.
Ngassa amesema, Kifungu Na. 3.0 cha Mwongozo huo kimewataka watoa mikopo hao pamoja na mengine kuwa na leseni na kutunza faragha za wateja wao.
“Ili mtoa huduma ndogo za fedha kuruhusiwa kutoa mikopo kidijitali anatakiwa kuwa na leseni ya kuendesha biashara ya Huduma Ndogo za Fedha chini ya Daraja la 2 chini ya kifungu Na. 16 cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na awe amefuata matakwa ya Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act) ya mwaka 2022 na kanuni zake."
Ameongeza kuwa, kufikia Novemba 14, 2024, Benki Kuu imepokea maombi 20
ya watoa huduma ya mikopo kidijitali (digital lending) ikiwemo taasisi na watu binafsi na tayari taasisi nne zimeshapewa leseni ya kufanya biashara hiyo.
“Na kwa kushirikiana na TCRA kuzifungia APPs 55 zilizogundulika kutoa mikopo mitandaoni bila kuwa na kibali cha Benki Kuu.” Alisema.
Ngassa amesema, mikopo ya mitandaoni ambayo hutolewa kupitia njia ya kidijitali kama vile aplikesheni za simu na tovuti imewavutia watu wengi kutokana na upatikanaii wake kuwa wa haraka hali ambayo imevutia watu ambao hawapati mikopo kirahisi kupitia benki au taasisi za kifedha rasmi kwa mfumo wa kawaida.
Awali wakati akifungua mafunzo hayo Kaimu Meneja wa Idara ya Huduma Ndogo za Fedha, Dickson Gama amesema,BoT inaendelea kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa thabiti, imara na stahimilivu ili kuwezesha shughuli za uchumi kuendelea kukua.
“BoT jukumu lake kubwa ni kusimamia huduma ndogo za fedha nchini hivyo kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari ambavyo ni kiunganishi kati ya Benki Kuu na jamii ya watanzania na dunia kwa ujumla, tunaamini kupitia nyie elimu hii itafika kwa urahisi kwa jamii yetu."
Ameeleza kuwa, mikopo ya mitandaoni imekuwa ni sehemu ya mfumo wa fedha kwani imerahisisha utoaji wa huduma za mikopo kwa urahisi zaidi na haraka.
Gama amesema, ukuaji huo wa haraka umesababisha changamoto kadhaa ikiwemo masuala ya kimaadili, riba kubwa gharama kubwa za mikopo na kukosekana kwa taarifa.
Pamoja na hayo amesema kutokana na changamoto hizo wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ili kufanya huduma hiyo kuwa na manufaa kwa wananchi na mtoa huduma kuidhinishwa na BoT.
Gama ametoa wito kwa wakopeshaji wa mtandaoni kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa na BoT ili kuepuka kufungiwa huku wakopaji wakisisitizwa kujiridhisha kwanza kama mkopeshaji amesajiliwa.