UVCCM Shanghai nchini China wampongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kurekodi mafanikio makubwa miaka minne ya uongozi wake

SHANGHAI-Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekutana na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM kutoka Shina la Shanghai, China.
Wana-CCM hao walifika kumpongeza Dkt. Mwinyi kwa mafanikio makubwa ya miaka minne ya uongozi wake, hususan kwa mchango mkubwa wa kuleta maendeleo ya kiuchumi, kuboresha sekta za kijamii, na kuimarisha diplomasia ya Zanzibar na nchi rafiki ya China.

Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Westin, Shanghai, ambapo Rais Dkt.Mwinyi alipata fursa ya kuzungumza na wana-CCM hao walioongozwa na ndugu Juma Athumani Sima, Mwenyekiti wa CCM Shina la Shanghai.
Katika salamu hizo, Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru Wana-CCM wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana, Shina la Shanghai kwa salamu zao za pongezi na kwa kutambua mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwashirikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi pamoja na wengine wasio raia, lakini wenye asili ya Kitanzania.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko katika mchakato wa kuandaa sera maalum itakayowanufaisha wanadiaspora kwa kuwapa hadhi maalum itakayowapa fursa mbalimbali zinazofanana na zile zinazotolewa kwa raia wa Tanzania.

Sera hii inalenga kuwapa wanadiaspora nafasi za kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kijamii, na maendeleo ya nchi kwa karibu zaidi, huku ikiwajengea mazingira bora ya uwekezaji, umiliki wa mali, na ushirikiano wa karibu na Serikali.
Rais Dkt. Mwinyi pia amewahimiza Vijana wa CCM kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news