VIDEO NA PICHA 36:Hawa ni binadamu au mashetani? Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR), kwa ushenzi wetu huu tunaanza kuitukana Serikali kweli? Si sawa

DAR-Kutokana na hali hii, Kamati za Kudumu za Bunge ya Bajeti na Miundombinu zimeshauri Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuweka mifumo ya ulinzi wa miundombinu ikiwemo ufungaji wa kamera za CCTV ili kudhibiti uharibifu wa miundombinu ya nyaya za umeme unaofanywa na watu wasio na nia njema na mradi huo.
Wakati wa ziara za kamati hizo kwenye reli hiyo jijini Dar es Salaam, ilielezwa kuwa hivi karibuni kumeripotiwa kusimama kwa treni mpya ya mwendokasi, huku sababu zilizobainishwa ikiwa ni uharibifu wa miundombinu ya nyaya za umeme, hivyo hakuna budi kuimarishwa ulinzi.
Katika ziara hiyo, ilibainika kuna upungufu na kasoro kadhaa katika miundombinu ya SGR zikiwamo za kiulinzi katika baadhi ya maeneo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso ameipongeza Serikali kwa kulijenga shirika na kulifanya kuwa la Kimataifa.

"TRC mmefanya kazi na jitihada kubwa sana na kulifanya Shirika letu kuzungumziwa na nchi mbalimbali, tumeshuhudia viongozi wa nchi za SADC na Afrika Mashariki wametembelea kuona mambo makubwa yaliofanyika" amesema Mhe. Kakoso.

Aidha, Mhe. Kakoso amewataka Wabunge kuendelea kuhimiza Serikali kufanya jitahada za kuikamilisha mradi wa SGR ili uweze kuunganisha nchi na maeneo mbalimbali ya nchi na nchi jirani.

"Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, tungekuwa hatuna dhati tungeweza kuliangusha Shirika lakini hoja zetu na michango yetu imeleta tija katika maendeleo haya, naomba tuendelee kupambana reli hii ikamilike " Amesema Mhe. Kakoso.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe. Oran Njeza amesema kuwa Tanzania imewakomboa nchi nyingi kisiasa sasa ni muda wa kuzikomboa nchi hizo kiuchumi kwa kuunganisha huduma za reli ili kurahisisha uvushwaji wa uchumi baina ya nchi hizo zote kwa maslahi mapana na kuinua uchumi wa Taifa.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Bi. Amina Lumuli amesema kuwa elimu na mafunzo kupitia semina ya wabunge itawawezesha kufahamu vyema dira ya Shirika ambayo imejikita katika kutoa huduma bora ndani na nje ya nchi.

TRC imeendelea kutoa huduma bora katika uendeshaji wa SGR ambapo ndani ya kipindi cha miezi minne ya uendeshaji imeweza kusafirisha zaidi ya abiria 800,000.

"Kupitia semina hii ,Wabunge watafahamu vyema dira ya Shirika ambayo imejikita katika kutoa huduma bora ndani na nje ya nchi, utoaji wa huduma ni endelevu na hata kwenye uendeshaji wa SGR tumekuwa na mafanikio makubwa" Amesema Bi. Amina

Bi. Amina ameongeza kuwa Shirika la Reli Tanzania linaongozwa na mpango mkakati ambao unaliwezesha Shirika kutekeleza majukumu yake ya kila siku katika kuwahudumia wananchi na kuchangia pato la Taifa.

Kamati za Bunge zimekuwa zikifanya ziara Mara kwa Mara kutembelea miradi ya TRC ili kuhakikisha ufanisi na ubora katika utekelezaji

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news