ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Novemba 15,2024 amejumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika ibada ya sala ya Ijumaa Msikiti wa Maungani Wilaya ya Magharibi B.
Akitoa salamu kwa waumini Alhaj Dkt. Mwinyi amewanasihi Vijana kuwathamini wazazi wao na kuwatendea mema ili kupata baraka za Mwenyezi Mungu.
Alhaj Dkt. Mwinyi amefahamisha ni wajibu na ni jambo jema kwa vijana ambao wazazi wao wako hai kuishi nao kwa huruma na upendo na kuwaombea dua wale waliotangulia mbele ya haki kwani kuna fadhila nyingi kwa kutekeleza jambo hilo.
Wakati huo huo, Alhaj Dkt. Mwinyi baada ya sala ya Ijumaa aliendeleza utaratibu wake wa kuwatembelea Wananchi na kuwajulia hali Wagonjwa katika maeneo mbalimbali.
Aliowatembelea leo ni aliekuwa Mbunge na Naibu Waziri Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mshauri wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Awamu ya Saba, Dkt. Maua Abeid Daftari anayeishi Beit Ras Wilaya ya Magharibi A.
Msanii Mkongwe wa sanaa za Filamu na Maigizo Zanzibar Bibi Mwanamwema Khamis Juma, maarufu Bi Njiwa.
Mwingine ni Bi. Halima Muhamed, Mjane wa aliekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama, Marehemu Borafya Silima wanaoishi Mwera Mtofaani.