Vodacom yaonesha kuimarisha Mtandao na Ujumuishaji wa Kifedha katika Ripoti ya Nusu mwaka ya 2024

DAR-Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc imetangaza matokeo ya kifedha ya nusu mwaka kwa kipindi kilichomalizika tarehe 30 Septemba 2024, yakionesha ukuaji mkubwa na juhudi za kuwawezesha Watanzania kupitia ujumuishaji wa kidijitali, uendelevu wa kimazingira, na upatikanaji wa huduma za kifedha.
Ripoti hiyo, iliyotolewa mwezi huu, inaonesha ongezeko la idadi ya wateja kwa 13.2%, ikifikia milioni 20.9, hivyo kuendelea kushikilia nafasi yake kama kinara katika sekta ya mawasiliano.

“Dhamira yetu ya ubunifu na kutoa huduma bora inaonekana katika uwekezaji na ukuaji wetu. 

"Tunaendelea kuwawezesha Watanzania kupitia uunganishaji jumuishi na mipango inayowezesha kila mmoja kufikiwa popote alipo bila kujali hali ya kipato chake,” alisema Philip Besiimire, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania.

Katika nusu ya mwaka huu, Vodacom imewekeza kiasi kikubwa katika miundombinu na uunganishaji, kwa kutumia TZS127.7 bilioni katika kuboresha na kupanua mtandao wake. 

Hii imesababisha kuongezeka kwa vituo vipya 259 vya 4G, hivyo kupanua upatikanaji wa intaneti na fursa za kidijitali katika maeneo yaliyokuwa hayajafikiwa awali.

Mafanikio mengine katika kipindi hiki ni pamoja na kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia M-Pesa. 

Mfumo wa M-Pesa umeendelea kukua, ukiwa na zaidi ya wateja milioni 6 wanaotumia huduma za mikopo, akiba, na bima. Katika kipindi hiki, mikopo midogo yenye thamani ya zaidi ya TZS1 trilioni ilitolewa, ongezeko la 30% ukilinganisha na mwaka jana, kusaidia biashara ndogo ndogo.

Vodacom pia imechangia katika utunzaji wa mazingira, ambapo imepunguza uzalishaji wa hewa ya CO₂ kwa tani 202 na kuokoa KWh 619,000 za matumizi ya umeme.

Juhudi za uwezeshaji wa kidijitali na kifedha pia zilijumuisha programu za elimu ya kifedha kama M-Koba, ambayo imefikia zaidi ya vikundi 12,000 na kuwasaidia wanawake ambao wanajumuisha asilimia 50 ya wanufaika. 

Miamala ya M-Koba ilifikia zaidi ya TZS1 trilioni, ikiwa ni ishara ya ongezeko la uelewa wa kifedha na utamaduni wa kuweka akiba.

Katika utendaji wa kifedha, Vodacom ilipata ongezeko la 19.1% la mapato ya huduma, yakichochewa na ongezeko la wateja na matumizi ya huduma za M-Pesa. Mapato ya M-Pesa yaliongezeka kwa 27.9%, wakati mapato ya data yalikuwa 16.7%, na data za kudumu zikiongezeka kwa 46.1%.

Vodacom inaendelea kujikita katika kuhakikisha kuwa inaongoza katika utoaji wa huduma bora za data kwa kutumia teknolojia za kisasa kama akili bandia, ili wateja waendelee kufurahia huduma. 

Uwekezaji unaoendelea katika miundombinu na ushirikiano na wadau utaendeleza uunganishaji, kusaidia ujumuishaji wa kifedha, na kuhimiza utunzaji wa mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news