Wabunge wa DRC wafanya ziara Wizara ya Mambo ya Nje

DAR-Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo amefanya mazungumzo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mtandao wa Maendeleo Endelevu ya Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ilipotembelea wizara Novemba 7, 2024 katika sehemu ya ziara yao ya kimafunzo nchini.
Katika mazungumzo hayo pande mbili zimeangalia maeneo ya ushirikiano kati ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania na DRC na kusisitiza umuhimu wa kuibua maeneo mapya yatakayongeza wigo wa ushirikiano.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Jimbo la Tanganyika-Kalemie, Mhe. John Banza Mbandu imeeleza dhamira ya kuendelea kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kupendekeza kuongezeka kwa safari za Ndege za Air Tanzania DRC hadi Kinshasa na Goma ambapo sasa safari zinaishia Lubumbashi, kupanua wigo wa ushirikiano katika miundombinu ya usafirishaji na kuongezwa kwa matawi mengine ya Benki ya CRDB nchini DRC itakayorahisisha biashara kati ya Wafanyabiashara wa Tanzania na DRC.

Aidha, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa miradi ya kimkakati inayoendelea kati ya Tanzania na DRC ikiwemo ule wa Treni kutoka Tanzania hadi Kindu lakini pia kwa mpango wa Reli ya Kisasa ya SGR kutoka Tanzania hadi Kindu itakayosaidia kusafirisha bidhaa kwa haraka ikiwemo usafirishaji wa madini kutoka DRC.

Kwa upande wake, Balozi Shelukindo ameipongeza Serikali ya DRC kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Manono hadi Kalemie, Jimbo la Tanganyika yenye urefu wa kilomita 446. ambayo ni kiungo muhimu cha kibiashara na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Ameeleza kuwa “Tanzania imekamilisha ujenzi wa Reli ya kisasa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma na kinafanya kazi. Ujenzi unaendelea katika hatua mbalimbali kwa vipande vingine kikiwemo cha Dodoma, Tabora hadi Mwanza na Tabora hadi Kigoma. Baadaye Reli inatarajiwa kujengwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania, Burundi na DRC kutoka Uvinza (Tanzania) – Gitega – Musongati - Bujumbura (Burundi) – Uvira hadi Kindu (DRC),” kitendo kitakachotatua moja ya mapendekezo yaliyoibuliwa.

Kamati hiyo pia imepongeza namna shughuli za Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania zinavyoendeshwa kwa weledi na nidhamu kufuatia ziara waliyoifanya bungeni hapo.

Ujumbe huu kutoka DRC upo nchini kwa ziara ya siku nne hadi Novemba 8, 2024 na unategemea kufanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam; Shirika la Reli la Tanzania, na kutembelea Bandari Kavu iliyopo Kwala Mkoa wa Pwani kwa lengo la kujionea jinsi Tanzania ilivyopiga hatua katika sekta ya usafirishaji; pamoja na kukutana na watendaji wa Benki ya CRDB.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news