ZANZIBAR-Wafanyabiashara wa Soko la Konde Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wametakiwa kudumisha usafi katika soko hilo ili kujiepusha na maradhi ya mlipuko katika eneo lao.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira na Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni katika ziara ya kutembelea soko hilo pamoja na makaazi ya wanajamii kwa lengo la kuangalia usafi katika maeneo hayo.
Mwenyekiti huyo amewataka wafanyabiashara hao kutokuuza biashara zao nje ya soko badala yake waingie ndani ya soko, kwani ni sehemu salama zaidi kwao.
Kwa upande wake katibu wa kamati hiyo ambaye pia ni afisa afya na mazingira wa halmashauri hiyo, Rashid Abdalla Seif amesema ni kuangalia hali halisi katika Soko la Konde pamoja kuangalia wauzaji wa bidhaa mbalimbali katika soko hilo ikiwemo mboga mboga,samaki,nyama pamoja na bidhaa nyingine.
Amesema, usafi ni jambo muhimu katika jamii hivyo ni vyema mfanyabiashara na mwanajamii anaweka usafi katika mazingira yake anayofanyia kazi pamoja na anayoishi.