PWANI-Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amewataka Wakandarasi wanaotekeleza Miradi ya TARURA ya ujenzi wa Barabara na Madaraja katika Mji wa Ikwiriri na Utete kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi ili kumaliza Mikataba yao kwa wakati.
Hayo yamejiri leo Novemba 8,2024 wakati wa ziara ya Ufuatiliaji (Monitoring) wa miradi ya Ujenzi na Matengenezo ya Barabara na Madaraja katika Mkoa huo wakati wa ziara ya Mtendaji Mkuu wa TARURA.
Mhandisi Seff akiwa katika Wilaya ya Rufiji alitembelea jumla ya Miradi Mitano (5) ya Ujenzi wa barabara na Vivuko/Madaraja na Makalavati katika Mji wa Ikwiriri na Utete.
Akiwa katika Mji wa Utete Mhandisi Seff amemtaka Mkandarasi NRST Ltd anayejenga barabara ya Utete-Kingupira Km.32 kwa kiwango cha changarawe kwa kutumia Teknolojia Mbadala (Mult-Enzymic Compound) kuongeza vifaa kwa mujibu wa Mkataba ili kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha kazi kwa wakati.
Vile vile, Mhandisi Seff ameridhishwa na kasi ya Mkandarasi RABCO Construction Ltd anayejenga Kalavati la Nambunju pamoja na kuchonga barabara ya Nyamwage ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 80.
Aidha, Mhandisi Seff amemtaka Mkandarasi MAC Contractor anayejenga Daraja la Mohoro kuongeza kasi ya utelezaji kwa kuzingatia Msimu wa Mvua unakaribia.
Mhandisi Seff aliahidi kurudi tena wiki ijayo ili kujionea hatua mbalimbali za Wakandarasi hao walizofikia.