Wamiliki wa ghorofa lililoporomoka Kariakoo wafikishwa mahakamani leo

DAR-Wamiliki wa jengo la ghorofa lililoporomoka katika Mtaa wa Mchikichini na Kongo Kata ya Kariakoo jijini Dar es Salaam wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Novemba 29,2024 wakikabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia.
Jengo hilo la biashara ambalo lilikuwa linahudumia idadi kubwa ya wafanyabiashara lililoporomoka Novemba 16,2024.

Wamiliki hao ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38) mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam.

Mbele ya mawakili watatu waandamizi wa Serikali Adolf Lema, Grace Mwanga na Erick Kamala mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, washtakiwa hao wamesomewa kesi hiyo kwa pamoja kwa kushindwa kutimiza majukumu yao na kusabashisha vifo vya watu 29 na majeruhi.

Mbali na hayo,wamiliki wawili wa jengo hilo wamepelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana huku mmoja wao ambaye ni Leondela Mdete (49) akipata dhamana.

Waliokosa dhamana ni Zenabu Islam (61), Mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38),Mkazi wa llala ambapo kwa pamoja walipewa masharti ya kuwa na wadhamini wawili kila mmoja mwenye barua za utambulisho.

Pia,kitambulisho cha Taifa na watatakiwa kusaini bondi ya shilingi milioni tano kwa kila mmoja.

Baada ya kuwasomea mashitaka yao Hakimu Mhini aliwaeleza washtakiwa kwamba hawatakiwi kujibu lolote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo huku upande wa Jamhuri ukidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Upande wa Jamhuri umeiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa, kesi imeahirishwa hadi Desemba 12,2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news