DODOMA-Jeshi la Polisi Tanzania limesema kuwa,katika kushiriki Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka 2024 litashirikiana na wadau mbalimbali kufanya Maadhimisho hayo katika Kanda Maalum ya Kipolisi Tarime Rorya ambapo jumla ya watoto 184 waliofanyiwa vitendo vya ukatili wameokolewa na jeshi hilo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi, DCP David Misime amesema kuwa,Jeshi la Polisi limeamua kuadhimisha siku hizo 16 katika Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya ambapo maafisa, wakaguzi na askari wengine wanaofanya kazi katika Madawati ya Jinsia na Watoto Tanzania Bara na Zanzibar sambamba na Wakaguzi wa Kata za Tarime Rorya, Serengeti na Butiama ambapo wataweka kambi.
DCP Misime ameongeza kuwa, shughuli watakazofanya wakiwa huko ni pamoja na kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto, ikiwemo madhara ya ukeketaji.
Amesisitiza pia tangu maadhimisho haya ya siku 16 yalipoanza Novemba 25, 2024 Jeshi la Polisi limefanikiwa kuokoa watoto zaidi ya 184 ambao walikuwa wameandaliwa kukeketwa mwezi wa Disemba 2024 na kwa kushirikiana na wadau wengine wamehifadhiwa sehemu maalum wakati hatua zingine za kisheria zikiendelea.