DODOMA-Jeshi la Polisi limewakamata na kuwahoji watuhumiwa wawili ambao ni watoto wa miaka 16 na miaka 12 kwa tuhuma za kuvunja vioo viwili vya Treni ya Mwendokasi (SGR) kwa kutumia mawe katika Kijiji cha Mnase, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi ambayo imefafanua kuwa watoto hao ni Erasto Michael Richard (16) na Hassan Ezekiel Ndahani ( 12) wakazi wa Kijiji cha Mnase.
Inadaiwa, walifanya tukio hilo wakati treni hiyo ikiwa inapita eneo hilo ikitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma.
Jeshi la Polisi limesema chanzo cha watuhumiwa hao kufanya kitendo hicho ni kupima uwezo wa spidi ya mawe na spidi ya treni hiyo kuona kama mawe hayo yangeweza kushindana na mwendo wa treni.
Aidha,jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi hasa wanaoishi maeneo ambayo treni inapita kuendelea kupeana elimu juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya treni,kwani ni kwa manufaa ya Watanzania wote.