DAR-Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe. Thomas Terstegen jijini Dar es Salaam leo Novemba 20,2024.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na kuendeleza mashirikiano katika kuboresha miundombinu ya Hifadhi ya Mwalimu Nyerere ili iweze kufikika vizuri, kuendelea kusaidia uhifadhi unaopatikana Ruvuma kupitia mradi wa GIZ pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali za uhifadhi katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Eliud Mtailuka, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Glory Mndolwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Taifa(NMT), Dkt Gwakisa Kamatula.