DAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, ameeleza kuwa, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, utakuwa wa haki, uwazi.
Pia, uchaguzi huo utazingatia misingi ya umoja na mshikamano, pamoja na falsafa ya R4 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa, Ofisi ya Rais TAMISEMI ilianzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kusogeza maamuzi karibu kabisa na wananchi.
Amefafanua kwa kusema kwamba, uchaguzi wa serikali za mitaa ni tofauti na uchaguzi mkuu, kwani mfumo wake unalenga wakazi ambao wanatambuana katika maeneo yao. Utambuzi huu wa wakazi unategemea wenyewe wakazi wa eneo husika.
Amesema hayo leo Novemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Waziri Mchengerwa ameendelea kwa kusema kwamba Bunge halikufanya marekebisho ya Ibara ya 145 na 146 ya katiba, wala tafsiri ya sheria inayosimamia uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hata hivyo, Bunge lilifanya marekebisho ya sheria inayosimamia mchakato wa chaguzi zinazoratibiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Vilevile Waziri Mchengerwa ameeleza kwamba, kumekuwa na propaganda za kisiasa kuhusu hali ya uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo amedai zinatolewa na baadhi ya watu ambao hawakuwa wamejiandaa vyema.
Amesema kuwa, uchaguzi huo ni shirikishi, na maandalizi yamehusisha vyama vyote vya siasa kwa njia ya vikao na mashauriano ya mara kwa mara na wadau wa vyama vya siasa.
Kuhusu kutotumika kwa vitambulisho wakati wa uandikishaji, Waziri Mchengerwa amesema, "Tungeweza kunyima haki za Watanzania walio wengi endapo tungeamua kuwa lazima kila mtu awe na kitambulisho ili aandikishwe.
"Tunatambua kwamba wananchi wengi, hasa wanaoishi kwenye vitongoji na vijiji, hawana vitambulisho.
"Hivyo, hatua hii imezingatiwa ili kila Mtanzania apate fursa ya kushiriki uchaguzi," amesema Mheshimiwa Mchengerwa.
Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mihayo Kadete amesema, uchaguzi wa serikali za mitaa unaongozwa na kanuni nne ambazo zinaelekeza namna gani uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika.
Amezitaja kanuni hizo kuwa ni kanuni ya uchaguzi wa mwenyekiti wa vijiji katika halmshauri za wilaya, kanuni ya uchaguzi wa mwenyekiti wa vijiji katika mamlaka ya miji midogo.
Kanuni nyingine, ni kanuni ya uchaguzi wa mwenyekiti wa serikali za mitaa katika halmashauri za miji na majiji pamoja na kanuni ya uchaguzi wa mwenyekiti wa vijiji katika mamlaka ya mji mdogo.
Kadete ameendelea kwa kusema kuwa, mgombea pekee atakayesalia katika uchaguzi atapigiwa kura ya ndio na hapana, kura za ndiyo zikiwa nyingi mgombea huyo atatangazwa kuwa mshindi na si kinyume chake.
Naye Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Mhandisi Andrew Kisaka amevitaka vyombo vya habari kutenda haki bila kuegemea upande wowote na kuvikumbusha kuwa vina wajibu wa moja kwa moja wa kuhamasisha wananchi kushiriki michakato ya uchaguzi ikiwemo kujitokeza kupiga kura.
Pia,kufuatilia mwenendo wa kampeni huku akionya waandishi kujiepusha kutoa mtazamo binafsi wakati wa kuhoji wagombea kipindi cha kampeni.
Uchaguzi wa serikali za mitaa ni fursa muhimu kwa wananchi kujitokeza na kuchagua viongozi watakaowakilisha maslahi yao katika ngazi za msingi.
Semina hiyo ya siku moja ambayo imeandaliwa na OR-TAMISEMI imeangazia zaidi kuhusu kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini.