DAR-"Yuko binti anaitwa Niffer (Jenifer Jovin) atafutwe aeleze nani alimpa kibali cha kuchangisha umma, amekusanya shilingi ngapi, amezipeleka wapi na kwa nini amefanya hivyo;
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametoa maagizo hayo kwa Jeshi la Polisi leo Novemba 18,2024 akiwa Kariakoo jijini Dar es Salaam alipofika kuona maendeleo ya zoezi la uokoaji linavyoendelea.
“Tumeona kuna watu wanaanza kuchangisha changisha huko pembeni, wanasema michango kwa ajili ya waathirika wa Kariakoo.
"Serikali imeendelea kupokea kwa watu wema wakileta misaada yao hapa, na walichokuwa wanaleta hapa ni maji, vyakula, biskuti kwa ajili ya waokoaji hatujaruhusu mtu mwingine yeyote huko nje kuanza kuchangisha Watanzania kwa ajili ya tatizo hili.
“Na hatukufanya hivyo kwa sababu Kamati ya Maafa iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu inao utaratibu wake, na kwa kuwa pia kuwa watu wako mbali wanahitaji kuchangia, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Waziri wa Nchi wameshatoa namba ya Benki Kuu ambayo ina Contol Number yake.
"Ambayo wewe popote ulipo unaweza kuchangia na ikienda inakuwa tayari imehesabiwa vizuri kama ambavyo tumefanya maeneo mengine, kwahiyo mtu mwingine yeyote haruhusiwi."
Niffer kupitia michango hiyo mpaka jana inadaiwa ameshakusanya zaidi ya shilingi milioni 37.
Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo amekagua muendelezo wa zoezi la uokoaji katika jengo lililodondoka eneo la Kariakoo jijini Dar es salaam na amesisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu hadi atakapotolewa mtu wa mwisho aliyekwama kwenye jengo hilo.
Aidha,Mheshimiwa Majaliwa amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wanamtafuta mmiliki wa jengo hilo ili aweze kusaidia kufahamu juu ya chanzo cha kudondoka kwa jengo hilo.
Pia ametoa wito wa watanzania kuacha kuchangisha Watanzania kwani Serikali inaoutaratibu wa utoaji wa misaada kupitia Kamati ya Maafa iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.