Waziri Mkuu azindua Kamati ya Uchunguzi kuporomoka kwa jengo Kariakoo

DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua Kamati ya Wataalamu ya Uchunguzi wa Jengo lililoporomoka katika eneo la Kariakoo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuchunguza chanzo cha tukio hilo pamoja na kufahamu ubora na uimara wa majengo yote yaliyoko Kariakoo.
Tarehe 16 Novemba, 2024, majira ya saa 3 asubuhi, ilitokea ajali ya kuporomoka kwa jengo la takriban gorofa tatu lililopo mtaa wa Agrey Kata ya Kariakoo, Jijini Dar es Salaam na kusababisha athari kubwa kwa watu na mali katika eneo hilo.

Akizungumza na kamati hiyo, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka ihakikishe kuwa inafanya uchunguzi wa kina, uwazi, haki na kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma.

“Fanyeni kazi hii kwa weledi, Taifa limewatuma nendeni mkaifanye kazi hii na mlete matokeo.”

Mheshimiwa Majaliwa amezindua kamati hiyo leo Novemba 21, 2024 katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, ambapo ameiagiza itekeleze majukumu yake kwa kufuata sheria, kanuni na maadili ya kazi.
Amesema mbali na kuchunguza jengo hilo lililoporomoka, pia kamati hiyo imeundwa ili kuchunguza majengo mengine yanayoendelea kutumika, katika eneo la Kariakoo, kuchunguza uimara wa majengo yanayojengwa, kuchunguza endapo taratibu zinafuatwa wakati wa ujenzi ikiwemo vibali, wakandarasi wenye sifa na usimamizi wa mamlaka husika wakati wa ujenzi.

Pia, Waziri Mkuu amesema madhumuni mengine ya kuundwa kwa kamati hiyo ni pamoja na kuchunguza endapo uboreshaji wa majengo unaofanywa Kariakoo unazingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na kubainisha majengo yote yaliyo katika hatari ya kuanguka na kupendekeza hatua za kuchukua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news