ZANZIBAR-Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar,Mhe.Tabia Maulid Mwita amezitaka taasisi za Serikali kuwashirikisha Maafisa Habari katika kazi zao ili wananchi waweze kupata taarifa kwa wakati.
Ameyasema hayo leo Novemba 28,2024 katika Ukumbi wa Shekh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni katika uzinduzi wa Jumuiya ya Maafisa Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICOO).
Amesema,kutowashirikisha maafisa hao katika kazi zao kunapelekea kuwakosesha wananchi kupata taarifa kwa wakati na kushindwa kujua shughuli maendeleo zinazofanywa nchini.
Aidha,amewataka maafisa ambao hawajajiunga katika jumuiya hiyo kujiunga ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema, kuwepo kwa jumuiya hiyo ni jambo muhimu, kwani itawawezesha maafisa hao kuwa na sauti moja na kujenga ushirikiano na taasisi nyingine.
Ameongeza kuwa, wakati Serikali ya Awamu ya Nane imehimiza suala la upatikanaji wa habari kwa wananchi,bado zipo baadhi ya taasisi hazifanyi kazi ipasavyo na kupelekea wananchi kukosa taarifa muhimu kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Ikulu na Msemaji Mkuu wa Serikali,Charles Hillary amewaasa maafisa wa habari kutobweteka na badala yake kujitahidi kufanya kazi kwa bidii ili wananchi wapate taarifa hizo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya Maafisa wa Habari na Mawasiliano Zanzibar,Makame Utari amesema lengo la kuwepo kwa jumuiya hiyo ni kuwaweka pamoja Maafisa wa Habari wote wa Serikali na kushirikiana ili kufanya kazi kwa weledi.
Amesema,jumuiya hiyo imefanikiwa kufanya ziara katika taasisi mbalimbali kujitambulisha na kujenga mahusiano na maafisa wa ndani na nje.
Aidha,amefahamisha kuwa jumuiya imefanikiwa kusajili wanachama 98 ambapo licha ya usajili huo bado inakabiliwa na baadhi ya changammoto ikiwemo uelewa mdogo kwa baadhi ya watendaji kuhusu majukumu ya Maafisa Habari, pamoja na ukosefu wa ofisi ya kufanyika kazi.
Aidha,ameongeza kuwa kuna mabadiliko ya kasi ya teknolojia, hivyo ni vyema kutolewa kwa mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa hao ili waendane na mabadiliko hayo.
Uzinduzi wa jumuiya hiyo unaenda sambamba na mafunzo ya maafisa habari ambayo yatafanyika kwa siku tatu baada ya uzinduzi huo.