Wengi walidhani hatutaweza, lakini haya tunayofanya ni salamu tosha-Rais Dkt.Mwinyi

NA GODFREY NNKO

"Wengi walidhani hatutaweza, lakini haya tunayofanya ni salamu tosha, tumeahidi na tumetekeleza na tutaendelea kutekeleza,na mengi bado yanakuja;
Hayo yalisemwa Novemba Mosi,2024 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi wakati akifungua skuli mpya ya ghorofa tatu ya Sekondari ya Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini kisiwani Pemba.

Uzinduzi huo ulikuwa ni sehemu ya mafanikio ya kihistoria katika Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi, kwani ndani ya miaka minne ametekeleza mengi katika Sekta ya Elimu.

Rais Dkt.Mwinyi ambaye aliapishwa Novemba 2,2020 amekuwa si kiongozi wa maneno mengi, bali mtekelezaji wa miradi na yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ustawi bora wa wananchi na Zanzibar kwa ujumla.

Ikumbukwe licha ya kuwekeza katika miundombinu bora ya elimu, rasilimali watu katika sekta hiyo, pia uwekezaji huo umepaisha ufaulu katika ngazi mbalimbali.

Mathalani, katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025 ambayo ni zaidi ya shilingi trilioni 5.18, Serikali chini ya Rais Dkt.Mwinyi imeweka uzito mkubwa katika Sekta ya Elimu.

Sekta hii imetengewa zaidi ya shilingi bilioni 830 ili ziweze kuongeza kasi katika uwekezaji na uboreshaji wa elimu kote Unguja na Pemba.Bajeti ya Elimu imepanda kutoka shilingi bilioni 265.5 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi asilimia 212.6.

Uwekezaji wa namna hii ndiyo umewezesha uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi zote za elimu kupanda kutoka 535,467 mwaka 2020 hadi kufikia wanafunzi 620,609 kwa mwaka 2024.

Aidha, kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, ndani ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dkt.Mwinyi, wanafunzi zaidi ya 35,941 walirejeshwa shule.

Mapinduzi hayo makubwa katika Sekta ya Elimu ndiyo yanayotoa hamasa kwa watoto wengi kote Pemba na Unguja kwenda shule, kwani miundombinu na huduma shuleni ni za kisasa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, chini ya uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi madarasa 2,738 na shule za ghorofa 35 zimejengwa kote Unguja na Pemba.

Aidha, mambo yanazidi kuwa mazuri zaidi kwani kupitia bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi inajenga madarasa mapya 2,037 zikiwemo shule 26 za ghorofa.

Vilevile, bajeti hiyo iliyoshiba inajenga shule za chini 53 ambazo tayari ujenzi umeanza kote Unguja na Pemba.

Mbali na hayo, ukarabati wa shule 91 umefanyika ambapo asilimia 67 ya shule za msingi na asilimia 87 ya shule za sekondari kwa sasa zinaendeshwa kwa mkondo mmoja.
Hiyo ni tofauti na huko nyuma ambapo shule hizo zilikuwa zikiendeshwa kwa mikondo miwili.

Pia, mbali na Serikali kutoa ajira mbalimbali katika Sekta ya Elimu, imekuwa mstari wa mbele vile vile kwa kuajiri walimu 72 kwa upande wa mahitaji maalumu.

Serikali ya Awamu ya Nane, pia imejenga vyuo vya Amali vitano kote Pemba na Unguja vikiwa mahususi kuwajengea vijana uwezo ili waweze kujiajiri baada ya kuhitimu.

Uwekezaji na maboresho hayo yamekuwa na matokeo chanya kote Unguja na Pemba, hii ni kutokana na kupaisha ufaulu kwa ngazi zote.

Mathalani kwa upande wa wanafunzi wa vipawa na michepuo katika mtihani wa darasa la saba umeongezeka kutoka asilimia 5.5 mwaka 2020 hadi asilimia 27.5 mwaka 2023.

Aidha, ufaulu kidato cha pili umeongezeka kutoka asilimia 76.8 hadi kufikia 94.6 huku ufaulu katika kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 55.4 hadi asilimia 85.6 mwaka 2023.

Ufaulu kwa upande wa kidato cha sita kote Unguja na Pemba umeongezeka kutoka asilimia 96.2 hadi kufikia asilimia 99.6 mwaka huu.

Kwa uwekezaji huu katika Sekta ya Elimu Zanzibar, kikubwa tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi ili aweze kutekeleza zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news