DODOMA-Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, ameahidi kukaa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kujadili njia bora za kuwarahisisha Wasanii wanaoitangaza nchi nje ya mipaka kupata hati za kusafiria za kihuduma.
Mhe. Mwinjuma alitoa kauli hiyo Novemba 1, 2024, bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Tauhida Cassian.
Mhe. Cassian alieleza umuhimu wa wasanii hao kupatiwa hati za kusafiria za kihuduma, ili waweze kuiwakilisha Tanzania kwa ufanisi zaidi katika matukio mbalimbali ya kimataifa.
Katika majibu yake, Mhe. Mwinjuma alisisitiza kuwa, Serikali inatambua mchango wa wasanii katika kuitangaza nchi na kuchangia katika uchumi wa nchi, licha ya kuwa Idara ya Uhamiaji ambayo iko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ina jukumu la kutoa hati za kusafiria na kwakua wasanii si miongoni mwa wanufaika wa hati za kidiplomasia au za kihuduma hivyo suala hilo litafanyiwa kazi.