DAR-Uongozi wa Young Africans Sports ya jijini Dar es Salaam umemtambulisha kocha mpya, Sead Ramovic ambaye ni muumini wa mfumo wa 4-2-3-1.
"Ni heshima kubwa sana kuwa hapa kuifundisha Young Africans Sports Club, ni Klabu kubwa sana yenye wachezaji wenye vipaji vikubwa na ni fahari kuwaongoza kuendeleza mafanikio ya Klabu hii yenye mataji mengi," amesema Sead Ramovic
Ramovic akiwa na TS Galaxy ya Afrika Kusini kwenye mechi sita za ligi hakushinda mechi hata moja huku akitoka sare mbili na vipigo vinne.
Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 45 ameiongoza TS Galaxy kuvuna alama mbili tu huku timu hiyo ambayo ipo mkiani mwa msimamo wa ligi ikifunga magoli manne na kuruhusu nane.
Ramovic anachukua mikoba ya Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina ambaye pamoja na kocha msaidizi Moussa Ndaw uongozi wa klabu hiyo umevunja mkataba nao leo.
Sead Ramovic ni nani?
Alizaliwa Machi 14, 1979 mjini Stuttgart, Ujerumani Magharibi.
Pia, ni mchezaji wa zamani aliyecheza kama kipa ambapo safari yake ya soka ilianza kwenye Academy ya FC Feuerbach kabla ya kuzichezea klabu kadhaa za Ujerumani.
Miongoni mwa klabu hizo ni Stuttgarter Kickers, VfL Wolfsburg, Borussia Mönchengladbach na Kickers Offenbach.
Julai 2006, Ramovic alisaini mkataba na Tromsø ya Tippeligaen kabla ya kuhamia Sivasspor mwaka 2010.
Aidha,baada ya hapo alijiunga na FK Novi Pazar mwaka 2011, akiendelea kucheza kwenye Super League ya Serbia kisha akamalizia soka lake katika Klabu ya Strømsgodset IF ya Norway.
Sead Ramovic alitangaza kustaafu soka Mei 21, 2014 akiwa na umri wa miaka 35 baada ya kucheza jumla ya mechi 235, kuruhusu mabao 321 na kuweka clean sheets 64.
Katika hatua nyingine,safari yake ya ukocha ilianza katika Klabu ya FK Novi Pazar ambako alikuwa kocha msaidizi kati ya msimu wa 2015/16 hadi 2020/21.
Oktoba 1, 2021 aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa TS Galaxy FC ya Afrika Kusini.