ZANZIBAR- Zaidi ya shilingi milioni 900 zimetaifishwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) na kuwa mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na kupatikana kwa njia ya haramu.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari huko ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Kanali Burhan Zubeir Nassor amesema, zoezi hilo limefanyika kwa mujibu wa Sheria Namba 8 ya mwaka 2021 ya ZDCEA.
Amesema,mamlaka imetaifisha Kiwanja kilichopo Matemwe na Honda ya aina ya Click, vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 422,126, Saleh Khamis Basmani Mkaazi wa Chukwani Wilaya ya Magharibi B na Mke wake Dawari Abas Fakih na kusema mamlaka inaendelea kuchunguza mali nyingine zilizomo ndani na nje ya nchi.
Aidha, amemtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni Mohamed Abdalla Juma mkaazi wa Michenzani Wilaya ya Mjini ambaye ni Mtumishi wa Serikali katika Kada ya Sheria ambapo ametaifishiwa kiwanja kilichopo Bweleo Wilaya ya Magharibi B, chenye thamani ya shilingi milioni 35.
Ni baada ya kubainika anashirikiana na Saleh Khamis Basmani katika utakatishaji wa fedha na kuingiza simu zinazotumika kufanya uhalifu kutoka nchini Afghanistan.
Pia, amesema mamlaka imetaifisha gari aina ya Toyota na nyumba zilizopo Paje Wilaya ya Kusini zinazomilikiwa na Andrea Scoph Fres, raia wa Ujerumani zenye thamani ya shilingi milioni 518,926 mara baada ya kukamatwa na mashine ya kisasa ya kuoteshea bangi, Polo moja la Bangi pamoja na Shamba la Bangi huko Paje Mkoa wa Kusini Unguja.
Mbali na hayo Kanali Burhan amesema, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaendelea kuwatafuta wanaojishughulisha na dawa hizo ili kunusuru vijana na utumiaji wa dawa hizo.
Itakumbukwa mnamo Aprili 22, 2024 mamlaka hiyo ilitangaza kutaifisha mali haramu ya dawa ya kulevya ya Saleh Khamis Basman mkaazi wa Chukwani na mke wake Dawari Fakih zenye thamani ya shilingi bilioni 15.3.