DAR-Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam,Bi. Happy Geofrey amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ubungo na kufunguliwa Shauri la Uhujumu Uchumi namba 33707/2024.
Katika shauri hili,Bi.Happy anashtakiwa kwa kufanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha shilingi 69,939,500 ikiwa ni mapato ya ada ya taka na ulinzi shirikishi kupitia mfumo wa POS.
Kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 28(1) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Pia ameshtakiwa kwa kosa la kutumia madaraka yake vibaya Kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Mashtaka haya yalisomwa na waendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Wakili Florida Mutalemwa na Sophia Nyanda, mbele ya Mhe. Tumsifu Gideon Barnabas, Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Ubungo.
Kesi hiyo itakuja tena mahakamani Desemba 17,2024 kwa ajili ya kusomwa hoja za awali.