Ajali ya Karagwe yamsikitisha Rais Dkt.Samia, atoa maagizo kwa Jeshi la Polisi

DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha madereva wanaongeza umakini na kuzingatia sheria za barabarani.
Ni katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika kote nchini.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa agizo hilo Desemba 4,2024 katika taarifa yake ya kusikitishwa na taarifa za ajali iliyohusisha magari matatu katika Kijiji cha Kihanga Wilaya ya Karagwe Mkoa wa Kagera na kusababisha vifo vya watu saba na majeruhi tisa jana.

“Ninawapa pole familia, ndugu, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Fatma Mwassa, jamaa na marafiki.

"Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu marehemu wote wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka,” ameandika Rais Samia kupitia mitandao yake ya kijamii.

Pia,amewataka abiria na watumiaji wote wa barabara kutumia namba za simu za makamanda wa polisi wa mikoa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wanapoona viashiria vya uzembe na ukiukwaji wa sheria na alama za barabarani.

“Utekelezaji wa agizo hili uende sambamba na uhuishaji na uwekaji wa alama za barabarani kwenye maeneo hatarishi, pamoja na kuzingatia umbali na maeneo sahihi ya uwekaji wa vituo vya ukaguzi ili vionekane kwa urahisi zaidi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news