KILIMANJARO-Watu tisa wamefariki huku kadhaa wakijeruhiwa katika ajali iliyotokea Desemba 26,2024 majira ya saa 3:40 jioni katika Kijiji cha Kibaoni, Tarafa ya Tarakea Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro.
Ni baada ya magari mawili kugongana kwenye barabara kuu ya Moshi kwenda Tarakea mkoani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema, ajali hiyo ilihusisha gari la abiria la aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T959 CKU, lililotoka Tarakea kuelekea Moshi, kugongana na basi la abiria la aina ya Yutong lenye namba za usajili T620 DZQ, lililotoka Dodoma kuelekea Tarakea.
Amesema,gari la Noah lilikuwa limejaa abiria, na lilipogongana na basi hilo ambapo watu tisa waliokuwa kwenye gari la Toyota Noah walipoteza maisha.
Watu waliokufa ni pamoja na Mamasita Lowasa (27) mkazi wa Kamwanga, Damarisi Kanini Mwikau (22) mkazi wa Elast, KenyaPeter Alex Urio (38).
Pia, yupo Monica Joyce Mumbua (64), MkenyaEligatanasi Kanje (30) mkazi wa Tarakea na Hilda Francis Leberatus (24) mkazi wa Kikelelwa.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo,mili mingine ya watu watatu haijatambuliwa hadi sasa.
Aidha, mtembea kwa miguu mmoja ambaye alijeruhiwa katika ajali hiyo amepelekwa katika Hospitali ya Huruma, Wilaya ya Rombo kwa matibabu. Hali yake bado haijafahamika.
Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa ajali ilitokana na uzembe wa dereva wa gari dogo la abiria Toyota Noah ambaye alijaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari ya kutosha.
Mili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma, Wilaya ya Rombo, kwa ajili ya uchunguzi wa kimatibabu na taratibu zingine.
Kamanda Simon Maigwa ametoa wito kwa madereva kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari zaidi ili kuepuka ajali zinazosababisha vifo na majeruhi