KAGERA-Watu saba wamefariki dunia na wengine tisa wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Kihanga katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Ajali hiyo imehusisha gari kubwa la mizigo aina ya Scania ambalo limeyagonga magari mengine mawili ya abiria yaliyokuwa yamesimama ambayo ni Hiace inayofanya safari zake kati ya Karagwe na Mutukula.
Sambamba na Coaster inayofanya safari zake kati ya Bukoba na Karagwe mkoani Kagera tarehe 3 Desemba 3,2024.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akisema chanzo ni uzembe wa dereva wa Scania.
Amesema,dereva huyo alikuja akiwa na mwendo mkali akayagonga magari hayo mawili yaliyokuwa na abiria ambayo yalisimama yakiwa yanakaguliwa na maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji kwenye eneo la ukaguzi
“Katika vifo hivyo saba kuna wanawake wanne, mwanaume mmoja na watoto wawili, kwenye majeruhi kuna wanaume wanne na wanawake watano.
"Chanzo ni uzembe wa dereva, kama ingekuwa mfumo wa breki umefeli asingeumaliza mteremeko na kona zilizo karibu na eneo la ajali, pia kuna vibao vinaonesha simama ukaguliwe.
“Ni wazi baada ya kumaliza mteremko hakuchukua tahadhari za barabarani, chanzo ni uzembe tu kutochukua tahadhari."
Aidha,Kamanda huyo ametoa rai kwa madereva kutambua hizo barabara sio zao pekee kwani wanatumia na watumiaji wengine.
"Kulikuwa na haja gani ya dereva kuja na spidi aliyokuja nayo? Ukiangalia madhara ya Hiace aliyoigonga ni ishara alikuwa spidi kali sana.
"Nasikia ametoroka haitomsaidia, ajisalimishe mwenyewe kabla hatujampata, tuna mkono mrefu hawezi kutukimbia akasalimika,"amesisitiza Kamanda Chatanda.