Anayesafiri kutoka Kigoma kwenda Dodoma kwa kutumia baiskeli kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita awasili Manyoni

NA RESPICE SWETU

MKAZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Wenceslaus Luyaga anayesafiri kwa kutumia baskeli kutoka Kasulu mkoani Kigoma kwenda Dodoma kuunga mkono juhudi za Rais wa Awamu ya Sita,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo, amefika Manyoni.
Akizungumza wakati wa kuanza safari hiyo, Luyaga ambaye pia ni mwalimu wa Shule ya Msingi Junga iliyopo katika halmashauri ya mji wa Kasulu, aliitaja baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa ni pamoja na treni ya mwendo kasi, umeme, maji na ujenzi wa meli.

Luyaga mwenye umri wa miaka 34 anayejulikana pia kwa jina la Gadafi alisema, pamoja na kuunga mkono juhudi hizo, safari hiyo pia inabeba ajenda ya kuwahamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia, utunzaji wa mazingira na kushiriki katika utalii wa ndani.

Aidha Luyaga aliitaja filamu ya Royal Tour aliyoshiriki Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa miongoni mwa vichocheo vya kufanyika kwa safari hiyo.

Akiwa Manyoni Luyaga pamoja na kupokewa na viongozi wa wilaya hiyo, amepita katika baadhi ya miradi ikiwemo ya maji, afya, elimu na barabara na kuzungumza na wananchi.
Akizungumzia safari hiyo, mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobiasi Andengenye alimtaja Luyaga kuwa shujaa na mzalendo wa kuigwa na kumhakikishia usalama katika maeneo atakayopita.
“Nakuhakikishia utakuwa salama katika safari hiyo, nimewasiliana na viongozi wa mikoa na wilaya utakazopita mpaka mwisho wa safari yako,”alisema Andengenye alipokuwa akimuaga na kumkabidhi bendera ya Taifa.

Luyaga anatarajia kukamilisha safari hiyo ya kihistoria Disemba 9 kwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Dodoma kabla ya kupanda mti kwenye mji wa serikali ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu na maadhimisho ya sherehe za miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news