DODOMA-Askari wa Jeshi la Polisi wawili wamefariki dunia wakati wakifanya majibizano ya risasi na mtuhumiwa, Atanasio Malenda (30) ambaye walienda kumkamata usiku wa kuamkia Desemba 18,2024 katika Kijiji cha Msagali Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma ambapo mtuhumiwa huyo pia amefariki baada ya majibizano hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema, majira ya saa saba usiku wa Desemba 18,2024 huko katika Kijiji cha Msagali Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma Askari Polisi D/Cpl. Jairo Boniface Kalanda na Pc. Alfred John walifariki dunia.
Ni katika mapambano ya risasi wakati wakimkamata Atanasio Malenda (30) ambaye ni mkulima mkazi wa Kijiji cha Msagali aliyekuwa anatuhumiwa kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha.
Inadaiaa, mtuhumiaa alilkuwa amemjeruhi, Yohana Lameck na kumpora kiasi cha shilingi milioni.
Amesema,askari polisi hao wakiwa na wenzao walipata taarifa kuwa mtuhumiwa huyo aliyekuwa anatafutwa yuko nyumbani kwake katika Kijiji cha Msagali na walifika kijijini hapo na kutafuta uongozi wa kijiji na kuelekea nao nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.
"Mtuhumiwa huyo alitoka ndani na kuanza kuwashambulia askari na katika majibizano hayo ndipo vikatokea vifo hivyo.
“Mtuhumiwa Atanasio Maleda naye amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mapambano hayo."
Aidha, katika majibizano hayo Askari D/cpl. Msuka na raia mmoja anayefahamika kwa jina la Masima Nyau wamejeruhiwa na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.